" MBUNGE SIGRADA ANAVYOVUNJA MIIKO YA SIASA KWA MAENDELEO YA UMMA

MBUNGE SIGRADA ANAVYOVUNJA MIIKO YA SIASA KWA MAENDELEO YA UMMA

Katika hali inayoonesha kuwa siasa si uadui bali ni nyenzo ya kuwahudumia wananchi, Mbunge wa Viti Maalum (CHAUMMA) Mkoa wa Njombe, Mhe. Sigrada Mligo, ameweka kando vazi la chama na kuvaa vazi la utumishi kwa kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kijiji cha Lugenge katika harakati zao za kujikwamua kiuchumi.

Safari ya wakazi wa Lugenge kuelekea mapinduzi ya kilimo ilianza kama ndoto ya watu wanne tu—wakulima wa parachichi na matufaa—walioamua kuanzisha ujenzi wa jengo la kuhifadhia na kuuzia mazao. Leo hii, ndoto hiyo imekua na kuunganisha jumla ya wakulima 83 ambao kwa jasho na ridhaa yao, wamekwishawekeza zaidi ya Shilingi milioni 27 katika ujenzi huo.

Licha ya jitihada hizo kubwa, ukamilishaji wa ghala hilo uligonga mwamba kutokana na uhaba wa rasilimali, hali iliyowafanya wananchi kuomba msaada kwa wadau wa maendeleo. Katika kuitikia wito huo, Mhe. Sigrada Mligo alifika kijijini hapo akiwa na shehena ya mifuko 50 ya saruji, akithibitisha kuwa kazi ya Mbunge wa upinzani si kupinga kila hatua ya serikali, bali ni kuwa daraja la kutatua kero za wananchi kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, Bernadino  alibainisha kuwa kukamilika kwa ghala hilo kutakuwa mkombozi dhidi ya walanguzi ambao wamekuwa wakiwanyonya. Alisisitiza kuwa ghala hilo litakuwa kitovu cha masoko ya uhakika kwa mazao ya matunda ambayo yameupa Mkoa wa Njombe sifa ya kipekee kitaifa.

Akihutubia baada ya kukabidhi msaada huo, Mhe. Sigrada alitoa ujumbe mzito kwa wananchi na wanasiasa nchini. Alisisitiza kuwa wakati wa kampeni umekwisha, na sasa ni muda wa kuunganisha nguvu na serikali iliyopo madarakani ili kuwaletea wananchi maendeleo.

"Anayewaza siasa (wakati wa kazi) ni yeye, lakini sisi tuendelee kushirikiana kwenye jambo lolote na tuendelee na kazi. Mimi nina wadau wangu, na naamini nitakwenda kuwashirikisha ili tukamilishe ujenzi huu," alisema Mbunge huyo huku akipigiwa makofi.

Mhe. Sigrada alikumbusha kuwa mshikamano ndio siri ya mafanikio ya Taifa, na kwamba mbunge makini ni yule anayewatafutia wananchi wake ufumbuzi badala ya kusubiri kila kitu kifanywe na serikali kuu pekee.

Hatua hii ya Mhe. Sigrada Mligo inatoa somo jipya katika ulingo wa siasa za Tanzania: kuwa upinzani wenye tija ni ule unaosaidiana na serikali kujenga nchi, na si ule unaoweka vizuizi kwenye miradi ya maendeleo. Kwa kutoa mifuko hiyo ya saruji na kuahidi kutafuta wadau zaidi, amewasha taa ya matumaini kwa wakulima wa Lugenge ambao sasa wanaona ghala lao likikaribia kukamilika.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post