Utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 umeonyesha kuwa na tija ya kipekee katika kuimarisha sekta za ujenzi na uchukuzi nchini Tanzania.
Tume ya Taifa ya Mipango inafafanua kuwa lengo kuu la mpango huo lilikuwa ni kuimarisha miundombinu ya barabara, madaraja, na vivuko ili kuifungua nchi na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa kuelekea maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya mipaka.
Kutokana na nafasi ya Tanzania kama lango kuu la biashara kwa nchi za Zambia, Malawi, DRC, Burundi, Rwanda, na Uganda, ujenzi wa miundombinu imara umekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na kuongeza kasi ya biashara za kimataifa. Mafanikio haya yanajidhihirisha kupitia upanuzi wa mtandao wa barabara zinazopitika wakati wote ambazo zimeongezeka kutoka kilometa 36,361.95 mwaka 2021/2022 hadi kufikia kilometa 37,225.72 mwaka 2024/2025.
Katika upande wa ajira na ustawi wa jamii, mpango huu umetoa matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi kupitia ujenzi wa barabara za vijijini kwa kiwango cha changarawe. Ongezeko la barabara hizi kutoka kilometa 35,476.59 hadi kilometa 41,107 mwaka 2024/2025 limekuwa na mchango mkubwa kwa kuzalisha ajira 21,527 katika mwaka 2024 pekee.
Aidha, ustawi wa kampuni za ndani umeimarika ambapo ushiriki wa wazawa katika soko la ujenzi umepanda kutoka asilimia 35 hadi kufikia asilimia 40 ya thamani ya miradi yote nchini.
Maendeleo haya yameipelekea Tanzania kupiga hatua kimataifa kwa kupanda kutoka nafasi ya 60 mwaka 2022/2023 hadi nafasi ya 50 mwaka 2024/2025 katika ubora wa miundombinu kati ya nchi 189, huku sekta ya ujenzi ikichangia asilimia 12.8 katika pato la taifa na kufungua milango ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi.
Sekta ya uchukuzi pia imekuwa na mchango muhimu katika ustawi wa jamii ambapo mchango wake katika Pato la Taifa umepanda hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 7.1 ya awali.
Ukuaji huu unachangiwa na ongezeko kubwa la abiria wanaotumia usafiri wa reli, waliofikia zaidi ya milioni saba mwaka 2024/2025, pamoja na kuongezeka kwa wataalamu wa anga waliopatiwa mafunzo kutoka 279 hadi kufikia 1,123. Katika upande wa usafiri wa majini, ufanisi wa bandari umeongezeka ambapo idadi ya meli zimeongezeka na muda wa makasha kukaa bandarini umepungua kutoka wastani wa siku tisa hadi siku tano.
Vilevile, kuongezeka kwa wigo wa safari za ndege kumeimarisha sekta ya utalii na kusaidia wakulima kusafirisha mazao yanayoharibika haraka kwenda masoko ya nje kwa kutumia ndege maalumu ya mizigo, jambo linaloongeza kipato kwa jamii na kukuza ustawi wa taifa.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment