" TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO MKUBWA WA AFRIKA WA MITAMBO YA KILIMO

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO MKUBWA WA AFRIKA WA MITAMBO YA KILIMO

‎Tanzania inatarajiwa kuwa kitovu cha mijadala ya maendeleo ya kilimo barani Afrika baada ya kupangiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Afrika wa Uendelezaji wa Matumizi ya Mitambo ya Kilimo Endelevu, utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 3 hadi 6, 2026.

‎Mkutano huo utaenda sambamba na uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mkakati wa Taifa wa Uendelezaji wa Matumizi ya Mitambo ya Kilimo, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

‎Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkutano huo unaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO). Alisema lengo kuu la mkutano ni kutoa jukwaa la kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kuharakisha matumizi ya mitambo ya kisasa ya kilimo kwa maendeleo endelevu.

‎Chalamila amefafanua kuwa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Mitambo ya Kilimo utaweka mwelekeo mpya wa kuongeza tija, kupunguza kazi ngumu kwa wakulima na kuinua uzalishaji wa kilimo kupitia teknolojia za kisasa. Aliongeza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwahusisha Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi mbalimbali za Afrika pamoja na wadau wakuu wa sekta hiyo.

‎Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa FAO nchini Tanzania, Charles Tulai, amesema mkutano huo ni fursa muhimu kwa nchi za Afrika kujadili na kutafuta suluhu za pamoja kuhusu changamoto zinazolikabili bara hilo, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la kasi la idadi ya watu.

‎Tulai amebainisha kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na juhudi zake katika kuimarisha sekta ya kilimo na kuwatambua vijana kama nguvu kazi muhimu katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

‎Mkutano huo unatarajiwa kuimarisha dhamira ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya sekta ya kilimo kuwa chachu ya uchumi, ajira na ustawi wa wananchi nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post