Na Mapuli Kitina Misalaba
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Patrobas
Katambi, amewataka watumishi wa serikali na viongozi wa ngazi mbalimbali
kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia sheria ili
kulinda usalama na haki za wananchi.
Katambi ametoa maelekezo hayo leo wakati wa ziara yake
katika Manispaa ya Shinyanga, ambapo pamoja na mambo mengine amefanya mkutano
wa hadhara katika Uwanja wa Zimamoto Nguzonane mjini Shinyanga.
Amesema nchi ilitaka kuingia kwenye majaribu
yaliyosababishwa na watu wachache waliotaka kuhatarisha usalama wa taifa,
akisisitiza kuwa usalama wa taifa unahusisha haki ya wananchi kuishi kwa amani,
kuwa huru katika kufanya shughuli zao, kulindwa mali zao pamoja na kupata haki
zao za kiuchumi na kijamii.
Ameeleza kuwa ni wajibu wa serikali kuhakikisha
wananchi wanapata huduma za afya, miundombinu bora na haki ya kuchagua viongozi
wao kwa mujibu wa sheria, akibainisha kuwa masuala hayo pia ni sehemu ya msingi
wa usalama wa taifa.
“Hapa duniani ili tuweze kuishi tunawajibu wa kufuata
sheria kwa kuzitekeleza na kuzitii. Ndiyo maana sisi viongozi tumepewa jukumu
la kusimamia haki za wananchi, uhai wa wananchi, usalama wa wananchi na mali za
wananchi, tukizembea katika kusimamia hayo hakuna mtu ataweza kuishi kirahisi,”
amesema Katambi.
Aidha, amewapongeza wananchi wa Jimbo la Shinyanga
Mjini kwa kuendelea kuwa kielelezo cha kufuata taratibu na sheria, huku
akiahidi kuwa serikali itaendelea kuwahudumia kwa nguvu zote chini ya uongozi
wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katambi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama, akisisitiza kuwa viongozi wote
wanapaswa kuwahudumia wananchi kwa uaminifu na haki.
Amesema endapo kiongozi yeyote atabainika kula fedha
za wananchi, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila kusita.
“Ukipewa uongozi katika serikali hii ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania hakikisha unatimiza wajibu wako ukijua cheo ni dhamana.
Tusinyenyue mabega, tusitunishe matumbo, tufanye kazi kwa niaba ya Rais.
Hatutaki viongozi wenye maadili mabaya ambao wanakula rushwa na kuwanyima
wananchi haki zao za msingi,” amesisitiza.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment