Na Egdia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.
Mkuu wa wilaya ya Arusha Joseph Mkude amewakabidhi vibali maalum vijana, tayari kuanza zoezi la kukamata kila atakayetupa taka ovyo na kwa wafanyabiashara wasiosafisha maeneo yao.
Zoezi hilo limefanyika katika viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha, baada ya kumaliza mazoezi ya kutembea na kufanya usafi Kata ya Kaloleni, amewataka vijana kufanya kazi hiyo kwa weledi, kuepuka vitendo vya rushwa, upendeleo na kuepuka kubambikia wananchi kesi.
Aidha amesisitiza kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake, watendaji wa kata na maafisa afya kusimamia maeneo yao ipasavyo na kuwataka mawakala wa usafi kutekeleza majukumu yao kama mikataba yao inavyowaelekeza.
"Tutasimamia hili kwa ufasaha, nina imani kwa utaratibu huu tutafanikiwa kuweka mazingira safi kwa sababu hapa ndio lango la utalii, tutashirikiana na taasisi mbalimbali kununua mapipa ya kuwekea taka yatakayowekwa kila mahali" amesema Mkude.
Vilevile Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Iranqhe amesema wakati umefika taasisi zote iwe binafsi au serikali kukaa mguu sawa katika suala la kuweka mazingira safi na atakayebainika kukiuka utaratibu kuchukuliwa hatua stahiki.
"Sheria hii haitakuwa na msamaha kwa yeyote, ukikamatwa na kosa usipige simu jwa yeyote bali utatakiwa kuwajibika. Maafisa usafirishaji wa Jiji (Bodaboda) sasa kuweni makini maana baadhi yenu mmekuwa mkibebeshwa uchafu kwenda kuutupa mahali ambapo si sahihi, nawaagiza sasa mkawe mabalozi wazuri wa kutunza mazingira na kusafisha vituo vyenu".
Katika namna hiyo hiyo Mkuu wa kitengo cha udhibiti wa taka na usafi wa mazingira Jiji James Lobkok amesema vijana waliopewa vibali vya kukamata wachafuzi wa mji watafanya kazi kwa kubadilishana maeneo ili kuondoa mianya ya rushwa na upendeleo.
"Nimefarijika kwamba muamko wa kampeni ya weka jiji safi ni mkubwa, na sasa waendesha bajaji wameomba kupata kibali cha kukamata watakaotupa uchafu ovyo. Tukiunganisha nguvu kwa pamoja sisi ndio tutaongoza nchini kwa usafi badala ya Mkoa wa Kilimanjaro ambao umeongoza miaka yote" amesema Lobkok.



Post a Comment