" WANAWAKE, VIJANA ZAIDI YA 1,000 KUNUFAIKA MRADI WA NISHATI SAFI

WANAWAKE, VIJANA ZAIDI YA 1,000 KUNUFAIKA MRADI WA NISHATI SAFI


Na Mwandishi Wetu

Zaidi ya Wanawake na Vijana 1,500 wanatarajiwa kufaidika na mafunzo ya nishati safi  mradi ambao unatekelezwa baina ya serikali na Shirika la maendeleo ya kijamii (REDESO) kupitia vyuo sita za Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 27,2026 wakati wa Warsha wa kujadili mradi huo Afisa Mtendaji Mkuu wa REDESO, Abeid Kasaizi amesema mradi huo una nguzo kuu nne ambazo ni Kuandaa mitaala kwa ajili ya kozi fupi na ndefu,Kujenga uwezo wa vituo vya mafunzo hususan vile vilivyo chini ya VETA,  Kupanua wigo wa wanufaika na Kuhakikisha uendelevu wa mradi, ili baada ya muda uweze kujiendesha wenyewe kupitia mifumo ya VETA.

 Amesema kabla ya hapo walianza na mradi wa majaribio  uliowahusisha vijana na wanawake 500 ambaoo  Sasa wanapanua kufikia wanufaika 1,600.

"Mradi huu tuliubuni baada ya kutambua changamoto zinazowakabili wanawake na vijana katika jamii zetu. Wao ni sehemu kubwa ya jamii inayohitaji msaada na uwezeshaji. Wakati huo huo, dunia inahama kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu kama mafuta kwenda kwenye nishati safi Tulijiuliza: kwa nini Watanzania wengi, hasa wanawake na vijana, hawashiriki kikamilifu katika sekta hii mpya? alihoji.

Na kuongeza "Tuligundua kuwa kuna pengo la ujuzi . Ndipo tukabuni mradi unaolenga kuwajengea uwezo wanawake na vijana katika sekta ya nishati safi".

Amesema watawajenga uwezo vituo sita vya VETA kufundisha teknolojia za nishati safi, zikiwemo Majiko banifu, mifumo ya sola na Usafiri wa umeme  ikijumuisha uunganishaji, matengenezo na miundombinu ya kuchaji.

"Hatuishii tu kwenye ujuzi wa kiufundi pia tunatoa mafunzo ya ujasiriamali  ili wahitimu wasitegemee kuajiriwa pekee, bali waweze kujiajiri na kuanzisha biashara zao katika mnyororo wa thamani  wa mabadiliko ya nishati jadidifu",amesema.

Kasaizi amebainisha kuwa mradi huu unatekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mikoa ya  Dodoma, Mwanza, Singida, Dar es Salaam na Pwani.

"Hatukutaka kujikita Dar es Salaam pekee, kwa sababu mahitaji ya nishati hutofautiana kati ya mijini na vijijini. Kwa mfano, majiko banifu yana mahitaji makubwa zaidi katika maeneo ambayo bado yanatumia mkaa au kuni. Vivyo hivyo, usafiri wa umeme unaweza kuwa suluhisho muhimu kwa maeneo mengi ya mijini na pembezoni", amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda ya Dar es salaam wa VETA Wilhard Soko amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili ya kuandaa mitaala mipya na pia kutoa mafunzo kwa wakufunzi (Training of Trainers – ToT) yakilenga  kuwawezesha wanawake na vijana ili waweze kupata ajira katika sekta ya nishati jadidifu, si tu hapa Tanzania bali pia Afrika Mashariki na hata nje ya Afrika Mashariki.

 "Tunataka vijana wetu wawe na uwezo wa kufanya kazi kwa umahiri mkubwa katika sekta hii inayokua kwa kasi.Mradi huu umejengwa juu ya utafiti maalum unaoitwa Utafiti wa Soko la Ajira. Utafiti huu haukuwa wa kawaida tu, bali uliangalia kwa kina mapungufu yaliyopo kwenye mitaala na mafunzo yetu, ili kubaini ni ujuzi gani unahitajika katika sekta ya Green Energy",ameeleza.

Amesema mradi umewasaidia  kubuni mitaala inayozingatia umahiri ili wahitimu wetu wawe tayari kuingia moja kwa moja kwenye ajira.

"Tunatoa shukrani kwa REDESO na hasa International Development Research Centre (IDRC) kwa kufadhili tafiti hizi na kusaidia utekelezaji wa mradi huu. Kupitia ushirikiano huu, tunaimarisha uwezo wa taasisi zetu kufundisha wanawake na vijana katika sekta ya nishati jadidifu", amesema.



  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post