" HUU HAPA WASIFU WA MAREHEMU WILLIAM LUKUVI

HUU HAPA WASIFU WA MAREHEMU WILLIAM LUKUVI






Na. Meleka Kulwa- Dodoma

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa marehemu William V. Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 majira ya saa 1:00 asubuhi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu, kufuatia ugonjwa wa mshtuko wa moyo.

Dkt. Yonazi ameyasema hayo Machi 27,2026 wakati akisoma wasifu wa marehemu katika shughuli za maombolezo, ambapo alieleza kuwa taifa limepoteza kiongozi mahiri aliyelitumikia kwa bidii, ufanisi na uadilifu wa hali ya juu katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ubunge na uwaziri.

KUZALIWA

Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi alizaliwa tarehe 15 Agosti 1955 katika kijiji cha Mapogoro, Kata ya Idodi – Wilaya ya Iringa Vijijini, Mkoani Iringa.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alikuwa mwanasiasa mashuhuri alieshika nyadhifa mbalimbali za uongozi na aliesifika kwa ubunifu, uthubutu, uchapakazi, uzalendo, mwenye uwezo wa kujitoa na kujituma katika kazi na aliweka maslahi ya Taifa mbele na wakati wote aliamini katika matokeo chanya katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali. Alijulikana kwa mtindo wake wa kazi wa kutembelea maeneo ya miradi na kusikiliza kero za wananchi moja kwa moja, jambo lililosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali. Katika kudhihirisha uchapakazi wake, siku moja kabla ya umauti kumkuta, marehemu alihudhuria na kuratibu Serikali katika Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali ya Serikali.

ELIMU

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alipata elimu ya Msingi katika Shule ya Msingi Kitanewa kuanzia mwaka 1962 hadi 1970. Alijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) kuanzia mwaka 1974 – 1975 ambapo alihitimu na kutunukiwa Cheti cha Ualimu. Mwaka 1982- 1983 alijiunga na Shule ya Komsomol High School, Moscow nchini Urusi na kutunukiwa Stashahada ya Juu ya Sayansi ya Siasa (Advanced Diploma in Political Science). Alipata Shahada ya Masuala ya Kimatiafa na Diplomasia yaani Bachelor of Arts in International Studies and Diplomacy kutoka Washington International University kuanzia mwaka 1999 – 2001, na baadaye alijiendeleza kimasomo katika ngazi ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Huria Tanzania ambapo alihitimu na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Siasa mwaka 2008 – 2011.

KAZI NA SIASA

Marehemu William Vangimembe Lukuvi alianza safari yake ya kisiasa mwaka 1973 alipojiunga na Chama cha TANU akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tabora (TCC) na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama katika chuo hicho mwaka 1974 – 1975. Mnamo mwaka 1984 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Vikao vya umoja wa Vijana wa CCM katika Ngazi ya Wilaya hadi Taifa. Alichaguliwa kuwa Katibu wa Mkoa na Wilaya wa chama cha CCM mwaka 1980 – 1984. Vile vile, aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM mwaka 1993 – 1994. Aidha, Alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashuari Kuu ya CCM na Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Chama mwaka 2010 hadi sasa.

Marehemu William Vangimembe Lukuvi aliajiriwa kama Mwalimu katika Wizara ya Elimu kuanzia mwaka 1975 hadi 1980. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba kuanzia mwaka 1994 – 1995, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma 2006 – 2008 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam 2008 – 2010.

Katika uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi vya Siasa nchini uliofanyika mwaka 1995, Marehemu Lukuvi alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Isimani na hivyo kuwa mbunge wa kwanza wa jimbo hilo alilolitumikia kwa takribani miaka 30 hadi umauti ulipomkuta. Akiwa mbunge aliwahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuanzia Mwaka 2005 – 2010.

Katika maisha yake ya siasa, Marehemu Lukuvi aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara kwanza alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Vijana na Ajira mwaka 1995 – 2000, na baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu na Mnadhimu Mkuu wa Serikali (Chief Whip) kati ya mwaka 2000 – 2005, 2010 – 2015 na 2025 – 2026. Halikadhalika, Marehemu Lukuvi aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba, na Maendeleo ya Makazi kuanzia Januari, 2015 hadi mwaka 2022.

Aidha, mnamo Juni 2023, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua kuwa Mshauri wa Rais kuhusu Mahusiano ya Kisiasa na Kijamii.

MAFANIKIO KATIKA SEKTA ALIZOONGOZA KIPINDI CHA UTUMISHI WAKE

Akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu),

Alikuwa msimamizi mahiri wa shughuli za Serikali Bungeni na alifanikiwa kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na Bunge, jambo ambalo lilimfanya kuwa mmoja wa Mawaziri wenye ushawishi mkubwa katika awamu mbalimbali za uongozi, na kujenga daraja imara kati ya Serikali, Bunge na wananchi.

Alisimamia utekelezaji wa sera mbalimbali zilizolenga kuboresha ustawi wa wenye ulemavu akihamasisha ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika fursa za kiuchumi na ajira na kusisitiza kuwa kundi hili ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya taifa.

Alisimmamia kikamilifu Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma ambao hadi sasa umefikia wastani wa asilimia 93 na tayari Wizara 15 zimeshahamia katika mji huo na zinatoa huduma kwa umma kutoka hapo.

Alisimamia uimarishaji wa mifumo ya kisera kwa kufanya maboresho katika usimamizi wa maafa nchini ikiwemo Mfumo wa Taarifa wa kielektroniki wa Usimamizi wa Maafa (Disaster Management Information System – DMIS), hatua iliyosaidia kupunguza Athari za maafa nchini.

Alikuwa mstari wa mbele kwa kuhakikisha Wizara zote zinafanya kazi kwa ushirikiano ili kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuhakikisha ahadi za serikali kwa wananchi zinatekelezwa.

Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Alifanikiwa kutatua migogoro ya ardhi nchini kwa kuanzisha mifumo bora ya kutatua migogoro ya ardhi na kupeleka huduma bora na zilizo karibu na wananchi.

Alisimamia uanzishwaji wa mifumo ya kidijitali ya usimamizi wa ardhi iliyolenga kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi, hatua iliyosaidia kuongeza mapato ya Serikali.

Alisimamia utoaji wa hati miliki za ardhi zaidi ya 1,992,245 kwa Watanzania hatua iliyosaidia kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutumia hati hizo kama dhamana za mikopo.

Alifanikiwa kutenga ardhi yenye ukubwa wa ekari 224,439.4 kwa ajili ya uwekezaji kupitia Mipango Kabambe ya miji, mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya na Vijiji. Hatua hii ilisaidia kuongeza uwekezaji nchini na kutoa ajira kwa wananchi.

Akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM

Alianzisha mfumo wa mbio za mwenge kwa kushindanisha mikoa katika maandalizi, hamasa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mikoa husika. Suala hili lilileta chachu ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi na kuleta matokeo makubwa kwa wananchi.

Alibuni na kuanzisha mradi wa mabasi ya wanafunzi katika Mkoa wa Dar es Salaam jambo ambalo lilipunguza adha kubwa ya usafiri kwa wanafunzi wa Jiji la Dar es Salaam.

Akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma

Alifufua na kuimarisha kilimo cha mtama na kuanzisha shamba la ushirika la zabibu akishirikiana na benki ya CRDB ambapo mradi huo sasa unasimamiwa na Wizara ya Kilimo ukijulikana kama BBT (Bulding a Better Tommorow).

Alihakikisha kuwa mipango ya upanuzi wa mji wa Dodoma inazingatia sheria na taratibu za mipango miji ili kuzuia ujenzi holela, jambo ambalo lilikuwa ni msingi muhimu wa ukuaji wa Mji mkuu wa kisasa.

Alisimamia Ujenzi wa Chuo Kikuu cha UDOM, hatua iliyosaidia kuongeza udahili wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini.

FAMILIA

Enzi za uhai wake, Marehemu Lukuvi alifunga ndoa takatifu tarehe 28 Julai, 1990 na Bi. Germina Lukuvi katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Jijini Dar es Salaam na kujaaliwa kupata watoto watatu ambao ni Nobert William Lukuvi, Brown William Lukuvi na Anifisye Vanessa William Lukuvi.

Marehemu Lukuvi ameacha mjane, watoto watatu na mjukuu mmoja aitwae Donovan.


SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment

Previous Post Next Post