" MAADHIMISHO YA WIKI YA LULU SACCOS YAANZA RASMI MBEYA WANACHAMA WAHIMIZWA KUZINGATIA SHERIA ZA USHIRIKA

MAADHIMISHO YA WIKI YA LULU SACCOS YAANZA RASMI MBEYA WANACHAMA WAHIMIZWA KUZINGATIA SHERIA ZA USHIRIKA

Na Lydia Lugakila- Misalaba Media

Mbeya

Vyama vyote vya ushirika mkoani Mbeya vimetakiwa kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na masharti ya vyama vya ushirika pamoja na miongozo inayotolewa na Msajili wa Vyama vya Ushirika, ili kuhakikisha vinaendesha shughuli zake kwa ufanisi na kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Wito huo umetolewa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mbeya, Elia Richard, wakati akizungumza na Misalaba Media katika ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Lulu Saccos Ltd, yaliyofunguliwa rasmi Machi 10, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Tughimbe, na yanatarajiwa kuhitimishwa Machi 13, 2026.

Richard amesema kuwa wiki ya Lulu Saccos ni fursa muhimu kwa wanachama kukumbushwa na kusisitizwa kuzingatia mambo ya msingi ikiwemo sheria, kanuni na taratibu za ushirika pamoja na mafunzo wanayopatiwa, ili kuleta mabadiliko chanya ndani ya vyama vyao.

“Nasema haya kwa sababu kama mafunzo haya yanafanyika kila mwaka lakini hayazingatiwi, basi hayataleta faida inayotarajiwa,” alisema Richard.

Aidha, ameipongeza Lulu Saccos Ltd kwa ubunifu wake wa kuandaa maadhimisho hayo kila mwaka, ambapo wanachama hukutana na kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo, kufanya mikutano ya kujadili maendeleo ya chama pamoja na kurudisha huduma kwa jamii kupitia misaada na sadaka kwa wenye uhitaji.

Richard amehimiza vyama vingine vya ushirika mkoani Mbeya kuiga utaratibu huo wa kukutana na wanachama pamoja na kufanya shughuli za kijamii, huku akisisitiza umuhimu wa kuuboresha zaidi ili uweze kuleta manufaa makubwa kwa wanachama na jamii kwa ujumla.

Maadhimisho ya wiki ya Lulu Saccos yamekuwa yakifanyika mwezi Machi Kila mwaka na kuwakutanisha wanachama, viongozi, watendaji pamoja na wadau mbalimbali wanaoshirikiana na Lulu Saccos katika shughuli zake.

Katika kipindi hicho, wanachama hupata mafunzo mbalimbali yanayohusu usimamizi bora wa vyama vya ushirika pamoja na mbinu za kuboresha huduma za kifedha kwa wanachama ambapo pia chama hicho huandaa shughuli za kijamii kwa lengo la kurudisha sehemu ya mafanikio wanayoyapata kwa jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, mhe. Solomon Itunda, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ameipongeza Lulu Saccos kwa mchango wake katika kukuza kipato cha wanachama pamoja na kuonyesha moyo wa kusaidia jamii.


Mhe Itunda pia ameongoza harambee maalum kwa ajili ya tukio la kuwafariji na kuwasaidia watu wenye uhitaji, tukio ambalo linatarajiwa kufanyika ndani ya wiki hiyo ya maadhimisho.

Hata hivyo Mhe Itunda amesema kuwa hatua ya Lulu Saccos kushiriki katika shughuli za kijamii inaonyesha wazi utekelezaji wa kauli mbiu ya chama hicho inayosema “Nguvu ya Ushirika ni Umoja wa Wanachama.”

 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post