" WANAWAKE WA KAMPUNI ZA GAKI INVESTMENT NA EAST AFRICAN SPIRITS WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI SHINYANGA, WAMPONGEZA MKURUGENZI KWA KUZINGATIA USAWA WA KIJINSIA

WANAWAKE WA KAMPUNI ZA GAKI INVESTMENT NA EAST AFRICAN SPIRITS WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI SHINYANGA, WAMPONGEZA MKURUGENZI KWA KUZINGATIA USAWA WA KIJINSIA

Wanawake wafanyakazi wa kampuni za GAKI Investment na East African Spirits (Super Women GAKI Group) wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kufanya hafla maalum ya kusherehekea mchango wa wanawake katika jamii na mahali pa kazi, huku wakisisitizwa kujiamini, kujitegemea kiuchumi na kudumisha umoja.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo ni Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni hizo, Gladnes Gasper Kileo, ambaye amesema kuwa maadhimisho hayo ni ya kwanza kufanyika katika kampuni ya GAKI Investment na yataendelea kuwa utamaduni wa kila mwaka.

“Leo tunaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, na hili ni tukio la kwanza kufanyika katika kampuni ya GAKI Investment. Tukio hili litakuwa endelevu na ninaahidi kuwa mwakani nitalisimamia mwenyewe,” amesema Kileo.

Amesema kuwa wanawake wakipewa nafasi wanaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa katika sekta mbalimbali, akitolea mfano uwepo wa wanawake katika uongozi wa juu serikalini, biashara na taaluma nyingine ambazo hapo awali zilikuwa zikitawaliwa zaidi na wanaume.

“Kwenye siasa tuna Rais mwanamke, kwenye biashara wanawake tupo, hata kazi ambazo zamani zilionekana ni za wanaume kama uendeshaji wa mitambo au ufundi umeme, sasa wanawake wapo wengi. Hata ndani ya familia mwanamke anaweza kufanya kazi huku akisimamia familia, jambo ambalo si rahisi lakini linawezekana,” amesema.

Gladnes amewataka wanawake kuanza kwa kujiamini ili waweze kufikia malengo yao katika maisha.

“Kumtambua mwanamke anaweza kunaanza na kujiamini. Kila kitu kinaanza kwenye fikra zako. Ukiamini unaweza, utaweza kweli; lakini ukiamini huwezi, kamwe hautaweza. Jiwekee malengo na amini unaweza kuyafikia,” amesisitiza Gladnes.

Aidha amewataka wanawake kujitegemea kiuchumi ili wawe na sauti ndani ya familia na jamii.

“Mwanamke ukiwa na kipato chako unapata uhuru wa kufanya maamuzi. Mwanamke asiye na kipato mara nyingi hukosa sauti katika familia na hata kwenye jamii. Ni muhimu kila mwanamke ajitafutie kipato chake,” amesema.

Pia amewahimiza wanawake kudumisha umoja na mshikamano, akisema kuwa utengano unaweza kudhoofisha mafanikio yao.

“Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Shikamaneni, shirikianeni na pendaneni. Hata mkipishana mawazo kumbukeni kuwa lengo lenu ni moja na mtaweza kusonga mbele,” amesema Gladnes.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Super Women GAKI Group, Immaculate Temu, amemshukuru mgeni rasmi kwa ushauri na hamasa aliyotoa, huku akiahidi kuwa wanawake wa kampuni hiyo watazifanyia kazi nasaha hizo.

Temu amesema maadhimisho ya mwaka ujao yatafanyika kwa kiwango kikubwa zaidi na kwa ubunifu tofauti ili kuendelea kuwainua wanawake ndani ya kampuni.

Katika hafla hiyo pia kulikuwa na mada mbalimbali za kuwahamasisha wanawake. Mtoa mada Savela Andrew amewahimiza wanawake kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili waweze kufikia mafanikio binafsi na kusaidia familia zao.

“Wanawake tunatakiwa kujituma katika kazi, kwani kazi ni msingi wa maisha. Mwanamke anapofanya kazi kwa moyo wote anaweza kuhudumia familia yake na kujijengea heshima katika jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa wanawake wanapaswa kuwa na lugha nzuri kazini, kupendana wao kwa wao na kujithamini.

“Mwanamke lazima ampende mwanamke mwenzake. Pia tuwe wasafi na tujitunze. Usipojipenda na kujithamini, nani atakupenda?”.

Naye mfanyakazi wa GAKI Investment, Lucy Kimati, amezungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.”

Amesema mwanamke ana mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwa kuwa anasimamia familia na wakati huo huo kushiriki katika shughuli za uzalishaji.

Kimati pia amempongeza mkurugenzi wa kampuni hizo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wanawake.

“Kipekee kabisa sisi wanawake wafanyakazi wa GAKI Investment tunamshukuru sana mkurugenzi wetu kwa namna alivyotoa nafasi kwa wanawake. Katika kampuni hizi wanawake ni wengi, jambo linaloonesha kuwa suala la usawa wa kijinsia limezingatiwa,” amesema Kimati.

Maadhimisho hayo yamelenga kuhamasisha wanawake kujiamini, kushirikiana na kutumia fursa zilizopo ili kufikia maendeleo yao binafsi na ya jamii kwa ujumla.

Kampuni ya GAKI Investment Limited ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa wa viwanda mkoani Shinyanga, ikijishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji na biashara zinazochangia kukuza uchumi wa wakulima na kutoa ajira kwa wananchi.

Moja ya shughuli kuu za kampuni hiyo ni uchambuzi wa pamba (cotton ginning) ambapo hununua pamba kutoka kwa wakulima katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na maeneo ya jirani kisha kuichambua katika kiwanda chake kilichopo mkoani Shinyanga.

Mbali na uchambuzi wa pamba, kampuni hiyo pia inajishughulisha na uzalishaji wa mafuta yatokanayo na mbegu za pamba, pamoja na shughuli nyingine za viwandani zikiwemo uzalishaji wa mifuko ya plastiki ya kufungashia bidhaa na uwekezaji katika sekta ya biashara.

Kupitia uwekezaji huo, kampuni ya GAKI Investment imekuwa ikitoa ajira kwa vijana na wanawake wengi pamoja na kusaidia wakulima kupata soko la uhakika la zao la pamba.

Wakati huo huo, kampuni ya East African Spirits (T) Limited, ambayo pia inahusishwa na uwekezaji wa kundi hilo la kampuni, inajishughulisha na uzalishaji wa vinywaji vikali (spirits) vinavyotengenezwa viwandani na kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Kampuni hiyo huzalisha aina mbalimbali za bidhaa za vinywaji vikali zinazouzwa katika soko la ndani na nje, ambapo imekuwa miongoni mwa kampuni zinazochangia ukuaji wa sekta ya viwanda pamoja na mapato ya serikali kupitia kodi.

Baadhi ya bidhaa zinazozalishwa ni pamoja na: Goldberg, Hanson’s Lite, Diamond Rock, Hanson’s Choice na Basembi.

Uwepo wa kampuni hizo mkoani Shinyanga umeendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi kwa kutoa ajira, kusaidia wakulima wa pamba kupata masoko na kuongeza thamani ya mazao kupitia shughuli za viwanda.

Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni za GAKI Investment na East African Spirits, Gladnes Gasper Kileo, akizungumza na wanawake wafanyakazi wa kampuni hizo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. 

Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni za GAKI Investment na East African Spirits, Gladnes Gasper Kileo, akizungumza kwenye hafla hiyo.TAZAMA PICHA MBALIMBALI




 

Post a Comment

Previous Post Next Post