Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua madhubuti kunusuru hali za kiuchumi za wakazi wa Jiji la Mwanza kwa kushusha timu ya wataalamu mitaani, lengo likiwa ni kutoa elimu dhidi ya mikopo kandamizi maarufu kama ‘Kausha Damu’.
Kupitia kampeni kabambe ya ‘Zinduka, Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo’, BoT imedhamiria kukata mnyororo wa umaskini unaosababishwa na mikopo yenye riba kubwa na masharti ya kinyonyaji.
Kampeni hiyo, ambayo imeng'oa nanga Aprili 1, 2026, inatarajiwa kudumu kwa wiki tatu ikipenya katika kila kona ya jiji hilo. Lengo kuu ni kuwatahadharisha wananchi dhidi ya kujiingiza kwenye mikataba ya "kichocheo cha kufilisika" na badala yake kuwahimiza kutumia taasisi za kifedha zilizosajiliwa na zenye leseni halali kutoka Benki Kuu.
Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hiyo, Meneja wa Uchumi wa Tawi la BoT Mwanza, Issa Pagali, ameweka wazi kuwa elimu hiyo ni kinga dhidi ya madhara makubwa ya kijamii yanayotokana na ukopaji holela.
“Tunataka wananchi wazinduke. ‘Zinduka’ inamaanisha kutambua haki zako kisheria; ‘Usiumizwe’ ni kuepuka kabisa mikopo yenye masharti magumu yanayolenga kupora mali zako; na ‘Kopa kwa Maendeleo’ ni kuhakikisha kila shilingi unayokopa inakwenda kuzalisha na si kutumika kwa mambo yasiyo na tija,” alisisitiza Pagali.
Katika maeneo ya Buseru, Pasiansi, Nyakato National na Nyamongolo Center wilayani Ilemela, maofisa wa BoT wameonekana wakitoa elimu ya ana kwa ana, wakifafanua jinsi wakopeshaji wasio rasmi wanavyotumia mbinu za kisaikolojia na vitisho kuwapokonya wananchi mali zao. Elimu hiyo imejikita katika:
Kutathmini uwezo wa kurejesha: Kabla ya kuweka saini, mwananchi anapaswa kujua kama kipato chake kinamruhusu kulipa.
Kusoma masharti: Kuepuka mikataba ya siri na riba zilizojificha ambazo huishia "kukausha damu" ya mkopaji.
Madhara ya kisheria: Kuelewa hatua zinazoweza kuchukuliwa endapo mteja atashindwa kulipa, badala ya kudhalilishwa au kuporwa mali kinyume cha sheria.
Hali kadhalika, BoT imetoa onyo kali kwa watoa huduma za kifedha mkoani humo, ikitaka wafuate miongozo na masharti ya leseni zao. Imeelezwa kuwa taasisi yoyote itakayobainika kutoa mikopo inayoumiza wananchi au inayokiuka taratibu za kibenki itachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufutiwa leseni.
Baada ya kukamilisha kutoa elimu wilayani Ilemela, kuanzia kesho Jumatatu, Aprili 6, 2026, msafara wa elimu hiyo utahamia Wilaya ya Nyamagana ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki gizani kuhusu usalama wa fedha zake.
Kampeni hii ni mwendelezo wa mkakati wa kitaifa wa BoT wa kuimarisha uelewa wa masuala ya kifedha (Financial Literacy) nchini.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment