Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika nchini kote mwezi Machi 2026, huku mitandao mipya ya usafirishaji ikibainika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mafanikio hayo yanatokana na mkakati wa Mamlaka kujikita zaidi katika operesheni za mashambani na kwenye njia kuu za usafirishaji baada ya kuimarisha udhibiti bandarini na mipakani.
“Katika kipindi cha mwezi Machi 2026, tumekamata jumla ya kilogramu 1,983.31 za dawa za kulevya aina mbalimbali, pamoja na kilogramu 3,012.5 na lita 17,960 za kemikali bashirifu ambazo zingetumika kuzalisha dawa hizo,” amesema Lyimo.
Ameeleza kuwa ongezeko kubwa limeonekana katika ukamataji wa mirungi, ambapo pekee yake ilifikia kilogramu 1,267.12 sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo, operesheni hizo pia zimefanikiwa kukamata vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, zikiwemo aina za benzodiazepine na opioid kama vile tramadol na codeine, ambazo hutumika vibaya na kusababisha uraibu.
“Tumebaini kuwepo kwa mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya, ikiwemo kuficha kwenye mizigo ya nguo za mitumba, matunda kama maembe, pamoja na ndani ya vyombo vya usafiri ikiwemo mifumo ya hewa (AC) kwenye mabasi,” ameongeza.
Katika operesheni hizo, watuhumiwa mbalimbali walikamatwa katika maeneo tofauti nchini wakiwemo Twahilu Athuman (38), Mohamedy Mikidadi (37) na Ibrahim Mohamed (39), huku magari tisa, pikipiki 12 na bajaji moja vikikamatwa.
Mikoa iliyohusika na ukamataji huo ni pamoja na Pwani, Mwanza, Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Songwe, ambapo baadhi ya dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kuelekea Dar es Salaam.
Aidha, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na watuhumiwa 77 kukamatwa kuhusiana na makosa hayo.
Kamishna Lyimo amesema Mamlaka inaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi nyingine za udhibiti ili kuvunja mitandao hiyo mipya.
“Tutahakikisha tunachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya bila kujali hadhi yake katika jamii,” amesisitiza.
Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za wahalifu na kuendelea kulinda jamii dhidi ya athari za dawa za kulevya, hususan katika maeneo ya taasisi za elimu.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment