" MADHARA YA KIUCHUMI NA KISAIKOLOJIA: HASARA NI SH BILIONI 125 ,VILIO NA MSONGO WA MAWAZO

MADHARA YA KIUCHUMI NA KISAIKOLOJIA: HASARA NI SH BILIONI 125 ,VILIO NA MSONGO WA MAWAZO

 


Ripoti ya Tume ya Jaji Othman Chande imefichua pigo kubwa la kiuchumi lililolipata taifa kufuatia ghasia za Oktoba 29, 2025, huku mali zenye thamani ya shilingi bilioni 125 zikiteketezwa na kuporwa.

Katika hali inayoonyesha sekta binafsi ndiyo iliyobeba msalaba mzito zaidi, asilimia 71.2 ya hasara hiyo, sawa na shilingi bilioni 89, imewakumba watu binafsi, vituo vya mafuta, benki na vyama, huku mali za umma zikichukua asilimia 28.8 ya uharibifu huo.

Simulizi za kusikitisha za waathirika zimepamba ripoti hiyo, ikiwemo ya mstaafu mmoja aliyepoteza gari lake la biashara (Tipper) lenye thamani ya shilingi milioni 180 lililochomwa moto eneo la Kimara Temboni, ikiwa ni miezi miwili tu tangu alinunue kwa mkopo wa benki.

Vilevile, wajasiriamali wadogo na wa kati hawakubaki salama, ambapo mali za thamani ya shilingi bilioni 1.6 ziliporwa, huku mfanyabiashara mmoja wa simu Tegeta akieleza kupatwa na msongo mkubwa wa mawazo baada ya duka lake kuvamiwa na kuibiwa simu zote ambazo alikuwa amezichukua kwa mkopo.

Mbali na hasara ya kifedha, Tume imebaini athari kubwa za kisaikolojia na kijamii miongoni mwa wananchi.

Matukio ya vifo, ulemavu, na kupoteza ndugu yamesababisha msongo wa mawazo, huzuni, na hofu kubwa. Hali hii imewagusa hata watoa huduma za afya ambapo waganga na wauguzi walilazimika kufanya kazi saa 72 mfululizo bila mawasiliano na familia zao, jambo lililowapelekea baadhi yao kupoteza hamu ya kuendelea na fani zao.

Mfano mmoja wa kuhuzunisha ni kijana kutoka Shinyanga aliyepoteza uwezo wa kutembea baada ya kupigwa risasi ya mguu, hali iliyomfanya akose uhuru wa kwenda shuleni na kujihisi hana thamani.

Hata hivyo, Tume ilichukua hatua za dharura kwa kuwaunganisha watu 710 waliokuwa na uhitaji mkubwa wa msaada wa kisaikolojia na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, ambapo wote wamepatiwa huduma mikoani na wilayani mwao. 

Katika upande wa uchumi wa kitaifa, ripoti hiyo inaeleza kuwa Tanzania imebakiwa na kiwango chake cha kuaminiwa kukopesheka (B1) kwa mujibu wa Moody’s, huku uamuzi wa Rais Samia kuunda tume hiyo ukitajwa na Benki Kuu kama hatua muhimu ya kurejesha imani ya wawekezaji katika soko la fedha na utalii nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post