Na Lydia Lugakila- Misalaba MediaMbeyaShule ya Sekondari Sangu ni miongoni mwa shule kongwe na zenye heshima kubwa katika Jiji la Mbeya. Ilianzishwa mwaka 1961,huku baadhi ya watu maarufu ambao ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge wakiwa ni zao la shule hiyo.Kwa zaidi ya miaka 65, shule hiyo imeendelea kuwa kitovu cha elimu bora kwa kulea wanafunzi katika misingi ya taaluma, nidhamu na maadili mema. Historia yake inaonesha mchango mkubwa katika kuzalisha wahitimu waliolitumikia taifa katika nyanja mbalimbali, jambo linaloifanya kuendelea kuaminiwa na jamii.Katika kuendeleza mafanikio hayo, shule imefanya mahafali ya 42 ya kidato cha sita mwaka 2026, ambapo jumla ya wahitimu wapatao 130 walihitimu. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa elimu.Mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Patrick Mwalunenge, ambaye aliwakilishwa na Meya wa Jiji la Mbeya, Mheshimiwa Dormohamed Issa.Akisoma taarifa ya shule, Mkuu wa Shule, Bw. Jacob Msigwa, alieleza kuwa Sangu imeendelea kufanya vizuri kitaaluma, hususan katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2025.Alibainisha kuwa matarajio ya wahitimu wa mwaka 2026 ni kupata ufaulu wa daraja la kwanza na la pili kwa kiwango kikubwa, huku akisisitiza kuwa mwenendo wa ufaulu umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.“Ufaulu wetu umekuwa ukipanda kila mwaka, hivyo tuna imani kuwa wahitimu wa mwaka huu watafanya vizuri zaidi na kuvunja rekodi ya miaka minne iliyopita,” alisema Msigwa.Alifafanua kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya shule na jamii inayowazunguka, juhudi za walimu wenye weledi, pamoja na uboreshaji wa miundombinu.Hata hivyo, alieleza kuwa bado kuna changamoto za uchakavu wa majengo, upatikanaji wa maji na miundombinu ya umeme.Alisema shule inaendelea kuweka mkazo katika ukarabati wa miundombinu hiyo ili kuendana na hadhi yake.Aidha, alitaja hitaji la ukarabati wa bweni la wasichana unaokadiriwa kugharimu shilingi milioni saba, akisisitiza umuhimu wake katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kike.“Tufanye juhudi hizi ili kuwaokoa watoto wetu, hasa wa kike, wanaotembea umbali mrefu kufuata elimu,” alisisitiza.Aliwashukuru wazazi, bodi ya shule na wadau mbalimbali kwa kuendelea kuiamini shule hiyo, akisema:“Asanteni wazazi kwa kutuamini kuwa sehemu ya kujenga hatima ya watoto wenu.”Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule aliwapongeza walimu na wafanyakazi kwa kujituma kwao, huku akiwashukuru wazazi kwa ushirikiano mzuri, hususan katika kulipa ada kwa wakati.Akizungumza katika hafla hiyo, mgeni rasmi Mhe. Dormohamed Issa alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake katika kuboresha sekta ya elimu nchini.Pia alimpongeza Mhe. Patrick Mwalunenge kwa kumuamini kumwakilisha, na kueleza kufurahishwa na historia ya shule hiyo pamoja na mafanikio yake.Aliwahimiza wanafunzi kuweka nidhamu, kujituma na kuwa na malengo makubwa ili kufikia mafanikio ya juu kitaaluma.“Kuweni na nidhamu na jitihada; mtaweza kufikia daraja la kwanza na kufanya maajabu makubwa,” alisema Dormohamed.Vilevile aliwakumbusha wanafunzi kuthamini juhudi za wazazi wao, akieleza kuwa wengi wao wamejitolea kwa hali na mali kuhakikisha wanapata elimu bora.“Wazazi wameangaika sana kuwafikisha hapa mlipo; wengine wameuza mali zao. Waheshimuni wazazi na msikate tamaa,” aliongeza.Kwa niaba ya Mbunge, aliahidi kuendelea kushawishi upatikanaji wa misaada ili kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo.Hafla hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa jengo jipya la utawala, hatua iliyoboreshwa kwa kiasi kikubwa mazingira ya kiutendaji ya shule, kwani hapo awali shughuli nyingi zilifanyika katika vyumba vya madarasa.Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mbeya Mjini, Bw. Emmanuel Barnabas, alikabidhi televisheni kwa shule kama sehemu ya mchango wake kwa maendeleo ya elimu.Alieleza kuwa msaada huo ni utekelezaji wa ahadi yake, akisisitiza kuwa si kila mchango unapaswa kuwa vitabu pekee, bali hata vifaa vingine vina mchango mkubwa katika kujifunza.Barnabas alimpongeza Mkuu wa Shule, Jacob Msigwa, kwa uongozi wake mzuri na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa maendeleo ya shule.Kwa ujumla, mahafali hayo yameakisi historia, mafanikio na dira ya Shule ya Sekondari Sangu katika kuendelea kutoa elimu bora, huku yakitoa matumaini mapya kwa wahitimu wanaotarajiwa kuwa sehemu ya nguvu kazi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment