" ‎RAIS SAMIA ATOA MAAGIZO YA KUBORESHWA MASOKO YA MAMA LISHE, ASISITIZA AMANI

‎RAIS SAMIA ATOA MAAGIZO YA KUBORESHWA MASOKO YA MAMA LISHE, ASISITIZA AMANI





………..

‎Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali imejipanga kuboresha mazingira ya kazi kwa Mama na Baba lishe nchini ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija zaidi huku wakichangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

‎Rais Samia pia amesisitiza kuwa amani ni msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, akieleza kuwa bila amani hakuna shughuli yoyote ya maendeleo inayoweza kufanyika kwa ufanisi.

‎Amesema kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yana athari kubwa kwa shughuli za wananchi, akirejea hali ilivyokuwa wakati wa matukio ya uchaguzi ambapo shughuli nyingi zilisimama kwa muda.

‎Aidha amebainisha kuwa ni wajibu wa Watanzania kuendelea kulinda mshikamano wa taifa na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, huku akiipongeza sekta binafsi kwa mchango wake katika kukuza uchumi wa nchi.

‎Akizungumza Aprili 21, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba lishe, Rais Samia amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe kushirikiana na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha maeneo yote yaliyoombwa na kundi hilo yanatengwa na kuendelezwa kwa ajili ya shughuli zao.

‎Aidha amebainisha kuwa ni muhimu kwa mamlaka husika kuhakikisha Mama na Baba lishe wanapatiwa miundombinu bora itakayowawezesha kufanya kazi katika mazingira salama na yenye tija, huku akisisitiza matumizi ya nishati safi katika shughuli za upishi ili kulinda afya zao na watumiaji wa huduma zao.

‎Rais Samia pia amesema kuwa Wizara ya Afya inapaswa kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya lishe na usalama wa chakula kwa kundi hilo, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda afya ya walaji na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.

‎Aidha amebainisha kuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinapaswa kuweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa mitaji kwa Mama na Baba lishe ili waweze kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi.

‎Pia ameongeza kuwa Wizara ya Fedha inatakiwa kuweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria yatakayowezesha wafanyabiashara ndogondogo kunufaika na huduma za kifedha pamoja na kukuza mitaji yao.

‎Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema kuwa ni jukumu la taasisi za utafiti na wadau wengine kushirikiana kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu, akibainisha kuwa matumizi ya nishati hiyo ni muhimu kwa afya na mazingira.

‎Aidha amebainisha kuwa wakati wa maonesho ya kongamano hilo, teknolojia mbalimbali za uzalishaji wa nishati mbadala ikiwemo mkaa unaotokana na mabaki ya mazao ya kilimo zimeoneshwa, hatua ambayo imewasaidia wadau wengi kupata elimu kuhusu matumizi bora ya nishati ya kupikia.

‎Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mama Lishe Tanzania (UMALITA), Bi. Julieth Malata amesema kuwa Mama na Baba lishe wanamtambua Rais Samia kama kiongozi mwenye mchango mkubwa katika kuwawezesha kiuchumi na kijamii.

‎Amesema kuwa Rais Samia amekuwa chanzo cha matumaini kwa wajasiriamali wadogo, akiongeza kuwa sera na mipango yake imefungua fursa nyingi kwa wanawake, vijana na makundi maalum nchini.

‎Aidha amebainisha kuwa umoja huo unaendelea kujifunza kutoka kwa uongozi wake, wakiamini kuwa kupitia juhudi hizo wanaweza kufikia mafanikio makubwa zaidi katika biashara zao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mama na Baba Lishe wanaoshiriki Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe, katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Profesa Riziki Shemdoe mfano wa hundi ya Shilingi bilioni 94.158,250,400/= kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba lishe, lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima ya Malkia wa Nishati safi kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) Bi. Havijawa Omary katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akifurahia jambo na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwenye Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam, tarehe 21 Aprili, 2026

Post a Comment

Previous Post Next Post