" VYOMBO VYA HABARI VYATAJWA NGUZO MUHIMU KUKUZA MAADILI KWA VIONGOZI WA UMMA

VYOMBO VYA HABARI VYATAJWA NGUZO MUHIMU KUKUZA MAADILI KWA VIONGOZI WA UMMA



Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Elizaberth Komba, amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee na yenye nguvu kubwa katika kujenga na kuimarisha maadili katika jamii na kwa viongozi wa umma.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa umma pamoja na wadau wa vyombo vya habari, Komba alisisitiza kuwa ushirikiano endelevu kati ya pande hizo ni muhimu katika kuhakikisha maadili yanazingatiwa katika utekelezaji wa majukumu ya kitaifa.

Alisema vyombo vya habari si tu chanzo cha taarifa bali pia ni chombo chenye uwezo wa kuunda fikra na mitazamo ya jamii, hivyo vina wajibu mkubwa katika kupambana na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

“Vyombo vya habari vina nguvu kubwa sana, vinaweza kusaidia kujenga jamii yenye maadili mema au kuharibu endapo vitatumika vibaya,” alisema Komba.

Aliongeza kuwa kupitia taarifa mbalimbali zinazoripotiwa, wananchi wamekuwa wakipata uelewa kuhusu vitendo vya rushwa, huduma mbovu na mienendo isiyofaa ya baadhi ya viongozi, hali inayosaidia kuongeza uwajibikaji.

Komba alifananisha nguvu ya vyombo vya habari na kampeni za uhamasishaji zilizowahi kufanyika kuhusu UKIMWI, akisema kuwa hata watoto wadogo waliweza kupata uelewa mkubwa kutokana na ujumbe uliokuwa ukitolewa mara kwa mara.

“Tunaposema maadili yawe ni wimbo, tunamaanisha ujumbe huu uendelee kusikika kila mahali kupitia vyombo vya habari ili kuibadilisha jamii,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wanahabari kutumia taaluma yao kwa njia sahihi ili kuhakikisha wanalinda na kukuza maadili, akionya kuwa matumizi mabaya ya vyombo hivyo yanaweza kusababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Kwa upande wake, mtoa mada Shaban Shirima alisema viongozi wa umma wana wajibu wa kisheria wa kutangaza rasilimali na madeni yao ndani ya siku 30 baada ya kuteuliwa au kuchaguliwa.

Alifafanua kuwa viongozi pia wanatakiwa kutoa tamko la rasilimali na madeni kila mwisho wa mwaka pamoja na wanapoondoka madarakani, ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji.

“Sheria inatutaka kuhakikisha taarifa hizi zinawasilishwa kwa wakati na kufanyiwa uhakiki ili kubaini kama ni sahihi au la,” alisema Shirima.

Aliongeza kuwa Sekretarieti ina mamlaka ya kufanya uchunguzi pale inapobaini au kupokea taarifa za ukiukwaji wa maadili, hata bila kusubiri malalamiko rasmi kutoka kwa wananchi.

Shirima alisema endapo itathibitika kuwa kiongozi ametoa taarifa zisizo sahihi, hatua za kisheria huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria za maadili ya viongozi wa umma.

Aidha, alibainisha kuwa taasisi hiyo pia ina jukumu la kutoa elimu kwa umma, kufanya tafiti kuhusu hali ya maadili nchini na kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo vyombo vya habari katika kukuza uadilifu.

Kwa pamoja, wasemaji hao walisisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, viongozi wa umma na vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kujenga utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na maadili bora katika taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post