
Hekaheka za mashindano ya klabu barani Afrika yamefikia hatua ya lala salama, ambapo miamba ya soka inasaka tiketi ya kucheza fainali. Wikiendi iliyopita ilikuwa ya vuta nikuvute, huku gumzo kubwa likiwa katika miji ya Algiers nchini Algeria, Rabat (Morocco) na Tunis (Tunisia).
Katika makala haya, tunakuchambulia mechi za nusu fainali za Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup) na Ligi ya Mabingwa (CAF Champions League) ambazo zimeacha maswali mengi kuliko majibu kuelekea marudiano Aprili 17 hadi 19, 2026.
Utawala wa Mafarao nchini Algeria
Mabingwa mara mbili wa Kombe la Shirikisho, Zamalek SC ya Misri, wameweka mguu mmoja kucheza fainali ya michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi mwembamba lakini muhimu wa 1-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.
Huu ulikuwa ni ushindi wa kihistoria kwa miamba hiyo ya Cairo, kwani ni mara yao ya kwanza kabisa kuifunga Belouizdad na ni mara ya pili tu kupata ushindi katika ardhi ya Algeria kwenye mashindano ya kimataifa.
Mchezo huo uliopigwa Aprili 10, 2026 kwenye Dimba la Nelson Mandela jijini Algiers nchini Algeria, ulishuhudia wenyeji Belouizdad wakitawala sehemu kubwa ya mchezo na kumiliki mpira, lakini walishindwa kutumia nafasi walizotengeneza.
Zamalek wakionyesha uzoefu wao mkubwa, walicheza kwa tahadhari na kutumia mashambulizi ya kushtukiza ambayo yalionekana kuwa na hatari zaidi.
Bao pekee la mchezo huo lilipatikana katika dakika ya 28 kupitia kwa Juan Bezerra. Shambulizi hilo lilianzishwa na krosi ndefu kutoka kwa Ahmed Abou El Fotouh iliyotikisa ngome ya Belouizdad, na kumruhusu Bezerra kupiga shuti la karibu lililojaa wavuni. Licha ya jitihada za Belouizdad, ikiwemo shuti la Abderrahmane Meziane lililogonga mwamba, Zamalek walilinda uongozi wao hadi kipyenga cha mwisho.
Sasa, miamba hiyo ya Misri inajiandaa kwa mchezo wa marudiano jijini Cairo mnamo Aprili 17, 2026 ikiwa na faida ya bao la ugenini.
Maajabu ya ‘underdog’ dhidi ya mabingwa
Moja ya matokeo yaliyoshangaza wengi ni suluhu ya 0-0 kati ya wenyeji na mabingwa wa zamani wa Kombe la Shirikisho, USM Alger, dhidi ya wageni wa mashindano hayo, Olympique Safi ya Morocco.
Safi ambao wanashiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza, walionyesha nidhamu ya hali ya juu ya ukabaji na ustahimilivu mkubwa dhidi ya wenyeji wao.
USM Alger, waliobeba ubingwa huu miaka mitatu iliyopita kwa kuifunga Yanga SC, watailaumu teknolojia ya VAR na kukosa umakini.
Dakika ya 54, Zakaria Draoui alidhani amewapa wenyeji uongozi, lakini bao lake lilikataliwa baada ya mapitio ya video. Hali kadhalika, Hocine Dehiri naye aliona shuti lake la dakika za lala salama likikataliwa, jambo lililoongeza machungu kwa mashabiki wa USM Alger.
Safi sasa wanarudi nyumbani Morocco wakiwa na matumaini makubwa, wakijivunia kuvuka matarajio kwa kufika hatua hii ya nusu fainali katika msimu wao wa kwanza kushiriki Kombe la Shirikisho. USM Alger watalazimika kufanya kazi ya ziada ugenini ili kulinda heshima yao.
AS FAR Rabat yaandika historia mpya
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kulikuwa na “Derby” ya Morocco ambapo AS FAR Rabat walikutana na wapinzani wao wa nyumbani, RS Berkane. AS FAR walichukua hatua kubwa kuelekea fainali kwa kushinda 2-0 kwenye Dimba la Prince Moulay Abdellah jijini Rabat.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkali, hususan katika kipindi cha kwanza ambapo timu zote zilicheza kwa tahadhari. Hata hivyo, mambo yalibadilika katika kipindi cha pili. Ahmed Hammoudane alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 58, baada ya kutumia mpira uliorudi (rebound) kufuatia shuti la Youssef El Fahli kuokolewa na kipa Anas Zniti.
Berkane walijaribu kurudi mchezoni na kushambulia kwa nguvu, lakini matumaini yao yalizimwa katika dakika ya 80 wakati Khalid Ait Ouarkhane alipopiga shuti kali la chini akiwa nje ya eneo la hatari na kuihakikishia ASFAR ushindi wa 2-0.
Ushindi huu unaiweka AS FAR katika nafasi nzuri ya kurejea fainali kwa mara ya kwanza tangu walipochukua ubingwa wao wa pekee mwaka 1985. Mshindi wa jumla kati ya hawa wawili atacheza fainali na aidha Mamelodi Sundowns au Esperance de Tunis ambao jana Jumapili usiku nao walikutana katika mechi ya mkondo wa kwanza uliopigwa Dimba la Hammadi Agrebi jijini Tunis nchini Tunisia na kuchezeshwa na mwamuzi Mustapha Ghorbal kutoka Algeria.
Nini kinafuata?
Kutokana na matokeo haya, ni wazi kuwa timu za Misri na Morocco zinaendelea kutawala soka la klabu barani Afrika. Zamalek wanaonekana kuwa na mguu mmoja fainali kutokana na uzoefu wao wa kucheza nyumbani Cairo.
Hata hivyo, Belouizdad walionyesha kuwa wanaweza kutawala mchezo, na kama wataweza kuwa na umakini kwenye umaliziaji, bado wana nafasi.
Kwa upande wa USM Alger, suluhu ya 0-0 nyumbani ni matokeo ya hatari. Olympique Safi wamethibitisha kuwa wao si wa kubezwa, na mchezo wa marudiano nchini Morocco utakuwa mtihani wa kweli kwa ujasiri wao.
Katika Ligi ya Mabingwa, AS FAR Rabat wameonyesha kwanini wanaitwa ‘Al Zaeem’ (Viongozi). Ushindi wa 2-0 unawapa jeuri, lakini RS Berkane ni timu inayojulikana kwa kupambana hadi dakika ya mwisho, hasa wanapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Berkane Municipal.
Mashabiki wa soka barani Afrika wanapaswa kujiandaa kwa wikiendi nyingine ya kusisimua. Je, miamba ya zamani itasimama imara na kufuzu fainali au wageni kama Olympique Safi wataendelea kuandika historia? Jibu litapatikana uwanjani!
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment