Ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Ghasia za Uchaguzi wa 2025 imeweka wazi kuwa usalama wa taifa katika karne ya 21 umevuka mipaka ya matumizi ya silaha za moto na sasa unategemea zaidi usalama wa taarifa.
Kufuatia matukio ya ghasia yaliyochochewa na majukwaa ya kidijiti, Tume imesisitiza kuwa elimu ya kidijiti kwa wananchi si jambo la hiari tena, bali ni hitaji la lazima la kiusalama. Hii ni kutokana na ukweli kwamba taarifa potofu zinaweza kusambaa kwa sekunde chache na kuwafikia mamilioni ya watu bila kuchujwa, jambo linaloweza kuibua hasira na maamuzi ya kukurupuka yanayotishia utulivu wa nchi.
Moja ya mafunzo makubwa yaliyopatikana ni umuhimu wa kuwafundisha wananchi, hususan vijana ambao ndio watumiaji wakuu wa mitandao, namna ya kuthibitisha ukweli wa picha na habari kabla ya kuzisambaza.
Ripoti imebainisha kuwa mbinu za kisasa kama matumizi ya picha zilizochezewa (deepfakes) na Akili Unde (AI) zilitumika kama silaha za kisaikolojia kuaminisha umma uongo, kama vile uwepo wa makaburi ya halaiki. Hivyo, uwezo wa mwananchi mmoja mmoja kuchambua taarifa unatajwa kuwa ndio kinga ya kwanza dhidi ya propaganda zinazolenga kuibua vurugu na kuharibu miundombinu muhimu ya nchi.
Aidha, ujenzi wa utamaduni wa mazungumzo yenye staha mtandaoni umeelezwa kuwa nguzo muhimu ya mshikamano.
Tume ilibaini kuwa lugha za chuki, kejeli, na kaulimbiu za uchochezi zilizosambaa kwenye majukwaa ya WhatsApp, X, na TikTok zilichangia kwa kiasi kikubwa kuhamishia uhasama kutoka kwenye ulimwengu wa kidijiti kwenda kwenye maisha halisi.
Ili kuzuia hali hii isijirudie, kuna haja ya kuimarisha mifumo ya mamlaka kama TCRA katika kufuatilia viashiria vya hatari mapema, huku jamii ikihimizwa kutumia teknolojia kwa ajili ya maendeleo badala ya kuibomoa nchi.
Aidha ripoti imesema kuwa amani ya Tanzania itategemea uwajibikaji wa kila mtumiaji wa mtandao. Kila mwananchi anapaswa kutambua kuwa kila picha au ujumbe anaosambaza unaweza kuwa na athari kubwa kwa usalama wa taifa na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050.
Katika dunia inayozidi kuwa ya kidijiti, kulinda ukweli na maadili ya mawasiliano ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa teknolojia inabaki kuwa chombo cha kukuza demokrasia na kuimarisha umoja, badala ya kuwa chanzo cha maangamizi na migogoro ya kijamii.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment