" JAMES MBOWE AWATAKA VIJANA KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KWA UWAJIBIKAJI

JAMES MBOWE AWATAKA VIJANA KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KWA UWAJIBIKAJI

 

Mwanasiasa na aliyekuwa mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Hai, James Mbowe, ametoa wito kwa vijana nchini kuacha kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria kupitia mitandao ya kijamii.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa matumizi ya majukwaa ya kidijitali, Mbowe alisisitiza umuhimu wa kutumia mitandao hiyo kwa staha, heshima na uwajibikaji, akionya dhidi ya matumizi ya lugha chafu, matusi pamoja na vitisho vinavyolenga viongozi na wananchi kwa ujumla.

Alieleza kuwa badala ya vijana kutumia muda mwingi mtandaoni kushambulia watu na kusambaza kauli za kashfa, wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika shughuli za kujiongezea kipato na kuchangia kukuza uchumi wa taifa.

“Nitoe rai kwa vijana kujikita zaidi katika shughuli za kuwaongezea vipato badala ya kushinda mitandaoni wakishambulia watu na kutoa maneno ya kashfa kwa viongozi na wananchi,” alisema Mbowe.


Katika hatua nyingine, Mbowe aligusia taarifa ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lililobainisha kuwashikilia vijana 37 kwa tuhuma za makosa ya kimtandao. Kwa mujibu wa Jeshi hilo, operesheni inaendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua wote wanaokiuka sheria za matumizi ya mitandao.


Amesisitiza kuwa mitandao ya kijamii si uwanja wa kuvunja sheria, bali ni jukwaa muhimu linalopaswa kutumiwa kwa hekima, manufaa binafsi na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post