
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, amesisitiza kuwa ingawa Tanzania inathamini mchango wa mataifa mengine katika kushughulikia changamoto mbalimbali, nchi hizo zinapaswa kutambua na kuheshimu kuwa Tanzania ni taifa huru.
Akichangia hoja bungeni, Nnauye alitoa mwito kwa mataifa ya nje kutotumia changamoto za ndani kama fimbo ya kunyanyasa, kukandamiza, kutuonea, au kutudhalilisha, bali watumie fursa wanazopewa kushirikiana na nchi kwa misingi ya heshima, nidhamu, na upendo.
Alikumbusha kuwa uhusiano wa Tanzania na washirika wake umejenga kwa miongo kadhaa, hivyo changamoto za muda mfupi haziwezi kutumika kama kipimo kikuu cha msingi wa mahusiano hayo, akisisitiza kuwa mataifa yote, makubwa kwa madogo, yako sawa mbele ya sheria za diplomasia ya kimataifa.
Nnauye aliongeza kuwa ujenzi wa taifa ni mchakato wa kihistoria unaochukua muda mrefu na unaohusisha kupitia nyakati njema na mbaya, za furaha na huzuni.
Aliwapongeza marais wote wa Tanzania kwa jinsi walivyosimamia diplomasia ya nchi katika vipindi vyote vya misukosuko na raha, akimtolea mfano Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimama imara katikati ya mawimbi na kuonyesha uzalendo mkubwa.
Alieleza kuwa msimamo huo umepeleka salamu madhubuti duniani kwamba Tanzania ina uwezo kamili wa kushughulikia matatizo yake yenyewe, jambo ambalo limeendelea kumletea heshima kubwa Rais na taifa kwa ujumla katika nyanja za diplomasia ya kiuchumi na ulinzi.
Naye Mbunge wa Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu, aliunga mkono hoja hiyo kwa kueleza kuwa diplomasia ya Tanzania imeimarika kwa kiwango kikubwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kingu alifafanua kuwa misingi ya uhusiano wa kimataifa na sera ya mambo ya nje ya nchi imejikita katika msimamo wa kutofungamana na upande wowote, huku kipaumbele kikuu kikiwa ni kulinda mamlaka kamili ya nchi, usalama wa mipaka, pamoja na uhuru wa kisiasa wa taifa la Tanzania.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, alibainisha kuwa Tanzania si kisiwa na iko tayari kushirikiana na mataifa mengine kwa ajili ya maendeleo, lakini ushirikiano huo lazima uzingatie wivu wa kulinda nchi kwa sababu hakuna Tanzania nyingine.
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu, alitoa mtazamo mwingine wa kidiplomasia akitaka Tanzania iendelee kusimama na kuhesabiwa katika kupinga dhuluma na kutetea haki duniani.
Shaibu alihimiza taifa kusimamia uwajibikaji wa mataifa makubwa, hasa katika kutekeleza ahadi zao za kuhifadhi mazingira, kwa kuwa wao ndio wazalishaji wakubwa wa hewa ya ukaa inayoumiza mataifa yanayoendelea.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment