" REA YAMTAMBULISHA MTOA HUDUMA WA MAJIKO BANIFU KAGERA, WANANCHI KUNUFAIKA NA RUZUKU YA ASILIMIA 80

REA YAMTAMBULISHA MTOA HUDUMA WA MAJIKO BANIFU KAGERA, WANANCHI KUNUFAIKA NA RUZUKU YA ASILIMIA 80



📍 *Bukoba, Kagera* 


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umemtambulisha rasmi mtoa huduma, kampuni ya Burn Manufacturing Company Limited, kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Kanali Yahaya Ramadhani Kido, ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku kwa wananchi wa mkoa huo.


Utambulisho huo umefanyika katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa mkoa pamoja na wataalamu kutoka REA, ambapo ilielezwa kuwa kampuni hiyo itahusika moja kwa moja na usambazaji wa majiko hayo pamoja na kuhakikisha yanawafikia wananchi kwa bei nafuu kupitia utaratibu wa ruzuku uliowekwa na Serikali. Mradi huo unalenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, ambavyo vimekuwa na athari kubwa kwa afya za wananchi na mazingira.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Ramadhani Kido, ameipongeza REA kwa kuendelea kuibua na kusimamia miradi yenye tija kwa wananchi, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo utakuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za nishati ya kupikia zinazowakabili wananchi wengi wa mkoa huo. Amesema matumizi ya majiko banifu yatasaidia kupunguza magonjwa ya mfumo wa upumuaji yanayosababishwa na moshi, hasa kwa wanawake na watoto ambao ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya nishati zisizo safi.


Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa mradi huo una mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti ovyo, hali inayochangia uharibifu wa misitu na kuongeza kasi ya mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza kuwa Mkoa wa Kagera uko tayari kushirikiana na REA na wadau wengine kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio makubwa na kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Stephen Ndaki, ameishukuru REA kwa kufanikisha upatikanaji wa mradi huo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuokoa maisha ya wananchi na kuboresha mazingira yao ya kuishi. Amesema kuwa majiko hayo banifu yatasaidia kupunguza athari za kiafya zinazotokana na moshi wa ndani ya nyumba, pamoja na kuchangia juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.


Naye Mhandisi Mwandamizi kutoka REA, Deusdedith Malulu, amefafanua kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia. Ameeleza kuwa kupitia mradi huo, jumla ya majiko takribani 12,500 yatasambazwa katika Mkoa wa Kagera ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.


Ameongeza kuwa kabla ya ruzuku ya Serikali, jiko hilo lilikuwa likiuzwa kwa takribani shilingi 100,000, hali iliyokuwa inawafanya wananchi wengi kushindwa kumudu gharama hiyo. Hata hivyo, kupitia mpango huo, Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 80 kwa kila jiko, na hivyo kushusha bei hadi kufikia shilingi 12,450 kwa jiko moja, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wa kipato cha chini wanapata fursa ya kumiliki na kutumia majiko hayo.


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Kido, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwa kinara wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini na barani Afrika kwa ujumla. Amesema juhudi hizo zimeleta mwamko mkubwa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi na salama.


Amesisitiza kuwa Mkoa wa Kagera uko tayari kuunga mkono kikamilifu jitihada za Rais kwa kuhakikisha wananchi wanahamasishwa, wanapatiwa elimu sahihi, na wanachangamkia fursa ya kutumia majiko banifu. Amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kununua majiko hayo kwa bei ya ruzuku ili kuboresha afya zao, kulinda mazingira, na kuchangia katika maendeleo endelevu ya taifa.


 *Mwisho.*

Post a Comment

Previous Post Next Post