" SHEIKH MAKUSANYA AWAHIMIZA WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU NA WANANCHI KUENDELEA KUDUMISHA AMANI NA KUWAOMBEA VIONGOZI WA SERIKALI

SHEIKH MAKUSANYA AWAHIMIZA WAUMINI WA DINI YA KIISLAMU NA WANANCHI KUENDELEA KUDUMISHA AMANI NA KUWAOMBEA VIONGOZI WA SERIKALI

 Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba Media

Waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Shinyanga wametakiwa kuwaombea viongozi wa taifa pamoja na kuendelea kudumisha amani, upendo na mshikamano nchini.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 27, 2026 na Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Ismail Habibu Makusanya, wakati wa swala ya Eid Al-Adha iliyofanyika katika uwanja wa Saba Saba uliopo kata ya Kambarage Mjini Shinyanga.

Sheikh Makusanya amesema Waislamu wanapaswa kuwaombea viongozi wao akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi ya kuwatumikia wananchi kwa karibu.

Amesema ni muhimu kwa waumini kuendelea kufanya dua kwa Mwenyezi Mungu ili viongozi wawe na afya njema, hekima na uwezo wa kuendelea kuliongoza taifa katika misingi ya amani na maendeleo.

Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani nchini kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha migogoro na kuvuruga mshikamano wa kitaifa, huku akisisitiza umuhimu wa umoja na upendo katika jamii.

Katika hatua nyingine, Sheikh Habibu ametoa wito kwa waendesha vyombo vya moto kuzingatia sheria na usalama barabarani wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Eid Al-Adha, ili kuepusha ajali zinazoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.

Pia amewasisitiza madereva wa bodaboda kuepuka kubeba abiria zaidi ya mmoja maarufu kama “mishikaki”, akisema hatua hiyo itasaidia kulinda usalama wa wananchi na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.

Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Ismail Habibu Makusanya, akiongoza swala ya Eid Al-Adha katika uwanja wa Saba Saba Manispaa ya Shinyanga leo Mei 27, 2026.

Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Ismail Habibu Makusanya, akiongoza swala ya Eid Al-Adha katika uwanja wa Saba Saba Manispaa ya Shinyanga leo Mei 27, 2026.

Waumini wa dini ya Kiislamu wakishiriki swala ya Eid kwa pamoja leo Mei 27, 2026 mkoani Shinyanga.







 

Post a Comment

Previous Post Next Post