Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga wameeleza
wasiwasi wao juu ya hali ya amani katika jamii, wakibainisha kuwa ukosefu wa
ajira na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana vinaweza
kuhatarisha utulivu na mshikamano wa kijamii.
Wakizungumza na Misalaba Media Mei 1, 2026, wananchi
hao wamesema vitendo vinavyotokana na matumizi ya dawa za kulevya, ikiwemo
uporaji, ukabaji, unyanyasaji wa watoto pamoja na kuvunjika kwa familia,
vinaashiria dalili za kuporomoka kwa maadili na vinaweza kuathiri amani endapo
havitadhibitiwa mapema.
Baadhi ya wananchi hao, akiwemo Abdallah Rajabu, Hamis
Hasan, Devotha Mfoi na Kitenge Chubwa, wameeleza kuwa vijana wengi hujikuta
wakiingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na ukosefu wa ajira
pamoja na ushawishi wa makundi rika na marafiki wabaya, hali inayochochea
kujiingiza katika vitendo vya uhalifu kama ujambazi na ukabaji.
Wamesisitiza kuwa ili kulinda amani iliyopo, ni muhimu
kwa wazazi na walezi kuimarisha malezi na kufuatilia kwa karibu mienendo ya
vijana, huku wakijenga mawasiliano ya karibu yatakayowasaidia vijana kueleza
changamoto zao mapema kabla hazijawaathiri.
Aidha, wameitaka serikali pamoja na wadau wa maendeleo
kuongeza juhudi katika kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, pamoja na
kuanzisha na kuimarisha programu za mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali ili
kuwapatia vijana fursa mbadala za kujiajiri.
Kwa upande mwingine, wananchi hao wamehimiza jamii
kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa kuhusu wahusika
wa biashara haramu ya dawa za kulevya, wakiamini hatua hiyo itasaidia kudhibiti
vitendo vya uhalifu na kuimarisha amani katika jamii.
Kwa ujumla, wametoa wito kwa serikali, wazazi na jamii
kwa ujumla kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hizo ili kuhakikisha
amani, usalama na maendeleo vinaendelea kudumishwa katika Manispaa ya
Shinyanga.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment