" UWANJA WA KISASA CHALINZE WAFIKIA ASILIMIA 52, KUBEBA WATU 11,000

UWANJA WA KISASA CHALINZE WAFIKIA ASILIMIA 52, KUBEBA WATU 11,000

 Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze

Mei 12, 2026

Ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mpira unaojengwa kata ya Msoga, Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, umefikia asilimia 52 ya utekelezaji, huku ukitarajiwa kuchukua mashabiki takribani 8,000 hadi 11,000 baada ya kukamilika.

Uwanja huo unaotarajiwa kuwa miongoni mwa miundombinu mikubwa ya michezo mkoani Pwani, unalenga kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana pamoja na kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri ya Chalinze kupitia shughuli za michezo na matukio mbalimbali.

Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Pwani imefanya ziara ya kukagua mradi huo na kuridhishwa na kasi ya ujenzi, huku ikielezwa kuwa unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, alisema mradi huo ni sehemu ya mageuzi makubwa katika sekta ya michezo mkoani humo na unaonesha maendeleo chanya katika Halmashauri ya Chalinze.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema uwanja huo utakuwa na hadhi ya kisasa na utawezesha timu mbalimbali kufanya mazoezi na hata kuweka kambi.

“Tutakuwa na sports complex hapa, michezo mbalimbali, Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mwelekeo wa matumizi ya mapato ya ndani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia halmashauri zetu,” alifafanua Kunenge.

Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Ismail Bilali, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri imetenga zaidi ya Sh bilioni 2.2 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo, ambapo tayari Sh bilioni 1.202 zimeshatumika.

Alieleza kuwa hatua iliyopo sasa ni ujenzi wa majukwaa yanayozunguka uwanja, ambayo ni sehemu ya awamu ya kwanza ya mradi unaotekelezwa na mkandarasi Monmar and Son Co. Ltd.

Naye, Joackim Mkalazaki aliipongeza halmashauri kwa kuwekeza katika sekta ya michezo, akibainisha kuwa wanaomba kujengewa kiwanja cha mpira eneo la Stendi ya Chalinze ili kusaidia timu yao ya stendi ambayo tayari ipo.

     




Post a Comment

Previous Post Next Post