" WACHIMBAJI WADOGO MWAKITOLYO NA.6 WAIOMBA SERIKALI KUINGILIA MGOGORO WA LESENI

WACHIMBAJI WADOGO MWAKITOLYO NA.6 WAIOMBA SERIKALI KUINGILIA MGOGORO WA LESENI

Wachimbaji wadogo wa dhahabu katika eneo la Mwakitolyo Na.6, wilayani Shinyanga, wameiomba Serikali ngazi ya juu kuingilia kati mgogoro wa umiliki wa leseni unaoendelea katika eneo hilo, wakidai kunyanyaswa na kuzuiwa kufanya shughuli zao halali.

Ombi hilo limetolewa katika kikao cha pamoja kilichowakutanisha wachimbaji hao, ambapo walieleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya shughuli za uchimbaji katika eneo hilo na kulipa mirabaha ya Serikali bila kusumbuliwa, lakini hali imebadilika baada ya kujitokeza kwa mtu anayedai kumiliki leseni ya eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya kikundi hicho, Katibu wa Kikundi cha Wachimbaji Vijana Mwakitolyo Na.6, Mussa Joel Peme, alisema tayari wamefuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kusajili kikundi chao tarehe 22 Januari 2026 na kupata usajili namba SHYDC/CBO 3073 kwa ajili ya kuendesha shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu.

Alisema hatua hiyo ilitokana na maelekezo ya Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde, aliyoyatoa Desemba 22, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara katika eneo hilo, ambapo aliwataka wachimbaji kuunda vikundi ili waweze kupata leseni na kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

“Tumechoka kunyanyaswa, tunaomba Serikali ya juu ituangalie kwa jicho la huruma. Hili eneo tumelifanyia kazi kwa zaidi ya miaka 30, na tunaendelea kulipa mapato ya Serikali kupitia soko la madini la Mwakitolyo,” alisema Peme.

Wachimbaji hao walisema licha ya jitihada zao za kufuata sheria, bado wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na uhakika wa umiliki wa eneo hilo, jambo linalohatarisha ajira zao na kipato chao.

Kwa pamoja, walitoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Madini na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Shinyanga kuchukua hatua za haraka ili kutatua mgogoro huo na kuhakikisha haki inatendeka kwa wachimbaji wadogo.

Walisisitiza kuwa wako tayari kuendelea kufuata sheria na taratibu zote za nchi, lakini wanahitaji msaada wa Serikali ili kupata leseni halali na kuendesha shughuli zao kwa amani na usalama.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

Post a Comment

Previous Post Next Post