Wapiga Kura 222,218 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki kwenye uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Isimani lililopo Halamashauri ya Wilaya ya Iringa Mkoani Iringa na Kata 12 za Tanzania Bara.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele ameyasema hayo leo Mei 31, 2026 Mkoani Iringa wakati akisoma risala maalum kuhusu uchaguzi katika jimbo na kata husika utakao fanyika kesho Juni 01, 2026 na kusema kuwa jumla ya vituo 628 vya Kupigia Kura vitatumika.
“wapiga kura 89,753 wapo kwenye Jimbo la Ismani na wapiga kura 132,465 wapo kwenye kata 12 zitakazofanya uchaguzi mdogo na vituo 277 vipo kwenye Jimbo la Ismani na vituo 351 vipo kwenye kata 12 zitakazofanya uchaguzi mdogo.,”amesema Jaji Mwambegele.
Aidha, amesema Katika Uchaguzi huu, jumla ya wagombea 108 kutoka katika vyama vya siasa 17 wanawania nafasi wazi ya ubunge na udiwani katika maeneo niliyoyataja.
“Jimbo la Ismani lina wagombea 17 wa nafasi ya Ubunge ambapo kati ya wagombea hao wagombea nane (08) sawa na asilimia 47.06 ni wanaume na wagombea tisa (09) sawa na asilimia 52.94 ni wanawake. Kata 12 zinazofanya uchaguzi mdogo wa udiwani zina jumla ya wagombea 91 ambapo kati ya hao wagombea 61 sawa na asilimia 67.03 ni wanaume na wagombea 30 sawa na asilimia 32.97 ni wanawake.” alisema Jaji Mwambegele.
“Natumia fursa hii kuvikumbusha Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi kesho Juni 01, 2026 kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya zoezi la kupiga, kuhesabu na kujumlishia kura. Wasimamizi wa uchaguzi katika Jimbo na Kata husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.
Amesema, mawakala hao, wanawajibika katika kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za Uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
Jaji Mwambegele amesema vituo vitafunguliwa saa 01:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni na kwamba ifikapo muda wa kufunga kituo saa 10:00 kamili jioni, kama wapiga kura bado wapo kwenye mistari, mlinzi wa kituo atasimama nyuma ya mtu wa mwisho na zoezi la upigaji kura litaendelea hadi wapiga kura walio kwenye mstari watakapomalizika.
“Baada ya kumaliza kupiga kura, mpiga kura anatakiwa kuondoka eneo la kituo cha kupigia kura; na Mpiga kura awapo kituoni, anatakiwa kufuata maelekezo yote atakayopewa na karani mwongozaji wapiga kura,”amesema Jaji Mwambegele.
Kwa mpiga kura ambaye ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na taarifa zake zipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililopo katika kituo husika, lakini amepoteza kadi yake au kadi yake imeharibika, ataruhusiwa kupiga Kura kwa kutumia moja wapo ya vitambulisho cha Taifa NIDA, Leseni ya udereva au Pasi ya kusafiria (Passport).
Kata 12 zitakazo fanya uchaguzi ni Mzimuni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni; Zongomera, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama; Itilo, Halmashauri ya Mji Nzega; Ketare, Halmashauri ya Mji Tarime na Nyumbigwa, Halmashauri ya Mji Kasulu.
Nyingine ni Kata ya Kala iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi; Ziba, Halmashauri ya Wilaya Igunga; Kamsisi, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele; Nyamugali, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe; Namasakata Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru; Bwongera, Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Kibiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment