
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Essau Hossiana Ngoloka, pamoja na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe wakikabiliwa na kesi tatu zinazohusisha tuhuma za rushwa na uhujumu uchumi.
Mashauri hayo yamefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Buhigwe mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mheshimiwa Kitoki Mwakitalu, yakiwa na namba ECCO 11952/2026, ECCO 11953/2026 na ECCO 11969/2026.
Mbali na Ngoloka, washtakiwa wengine ni Idrisa Mussa Naumanga, Sopharete Matete, Jerry Leonard Mwakapemba, Zacharia Cosmas Ntambala, Joachim Ibrahim Rweshunge na Jesfan Fares Ntagata.
Wakili wa Serikali kutoka Kigoma akisoma mashtaka hayo mahakamani, alieleza kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, matumizi mabaya ya mamlaka na matumizi ya risiti ya EFD inayodaiwa kuwa ya udanganyifu.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanatuhumiwa kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2022. Upande wa mashtaka unadai kuwa waliandaa nyaraka mbalimbali za ukaguzi wa mradi na tathmini ya kazi za ujenzi wa canteen ya Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na kuidhinisha malipo ya shilingi 5,300,000 kwa kazi ambazo zinadaiwa kutokufanyika.
Katika shtaka la pili la matumizi mabaya ya mamlaka, kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, washtakiwa wanadaiwa kuidhinisha malipo ya shilingi 3,300,000 kwa fundi sanifu wa mradi huo huku wakifahamu kuwa kazi husika haikuwa imekamilika na hivyo malipo hayo hayakustahili kutolewa.
Shtaka la tatu linawahusisha na tuhuma za kutumia risiti ya EFD yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 20 ambayo upande wa mashtaka unadai ilikuwa ya udanganyifu kwa kuwa haikuwa imesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa canteen ya halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, tuhuma hizo zinahusiana na matukio yaliyodaiwa kutokea mwaka 2023. Mashitaka hayo pia yamesomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200 Marejeo ya mwaka 2022.
Washtakiwa wote wamekana tuhuma zinazowakabili na wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama.
Kesi hizo zinaendeshwa na mawakili James Mosi Nyarobi na Omary Juma kutoka TAKUKURU Mkoa wa Kigoma, na zimeahirishwa hadi Juni 9, 2026 kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja za awali baada ya kufunguliwa mahakamani Juni 1, 2026.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment