Serikali imekabidhi rasmi eneo la ujenzi wa Jengo la
Mama na Mtoto la ghorofa tano pamoja na Jengo la Maabara ya Kisasa la ghorofa
mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, mradi unaotarajiwa
kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 25 na kukamilika ndani ya kipindi cha miaka
miwili.
Makabidhiano hayo yaliyohusisha utoaji wa Hati ya
Makabidhiano ya Eneo la Ujenzi (Site Possession Certificate) yamefanyika Juni
5, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, yakifungua rasmi
utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kuboresha huduma za afya mkoani humo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo,
Mshauri Mwelekezi kutoka Kampuni ya Volumetric Arch Consultant Ltd, Berno
Batinamani, amesema mkandarasi ataanza rasmi kazi za ujenzi Juni 19, 2026 na
mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Amesema kukamilika kwa majengo hayo kutasaidia
kuongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kisasa za afya kwa wananchi wa Mkoa
wa Shinyanga na mikoa jirani, hususan katika huduma za afya ya mama na mtoto
pamoja na huduma za uchunguzi wa maabara.
Kwa upande wake, Meneja wa Mkataba wa mradi huo kutoka
Wizara ya Afya, Festo Mapunda, amemtaka mkandarasi kuhakikisha anatekeleza
mradi kwa ubora unaotakiwa, ndani ya muda uliopangwa na kwa kuzingatia thamani
halisi ya fedha za umma.
Mapunda pia amesisitiza matumizi ya nguvu kazi kutoka
Mkoa wa Shinyanga ili wananchi waweze kunufaika na fursa za ajira
zitakazotokana na mradi huo.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya AMAR Builders Ltd,
mkandarasi anayetekeleza mradi huo, Vipul Maran, amesema kampuni yake
imejipanga kikamilifu kuhakikisha kazi zote zinakamilika kwa wakati na kwa
kuzingatia viwango vya kitaalamu.
Amesema tayari maandalizi muhimu ya awali yamekamilika
na kwamba wataendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na mshauri
mwelekezi ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Shinyanga, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. John Luzila, ameishukuru
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea
kuwekeza katika sekta ya afya.
Dkt. Luzila amesema Jengo la Mama na Mtoto litakuwa na
uwezo wa kuhudumia wagonjwa 162 kwa wakati mmoja, hatua itakayosaidia kupunguza
msongamano wa wagonjwa na kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto
katika Mkoa wa Shinyanga.
Aidha, amesema Jengo jipya la Maabara ya Kisasa lenye
ghorofa mbili litasaidia kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa na vipimo
mbalimbali vya kitabibu, hivyo kuwapunguzia wananchi gharama na muda wa
kusafiri kutafuta huduma hizo katika maeneo mengine.
Ameeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za
Serikali za kuimarisha miundombinu ya afya nchini kwa lengo la kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora, za kisasa na zinazokidhi mahitaji ya wakati.
Wadau waliohudhuria hafla hiyo wameeleza matumaini yao
kuwa mradi huo utakuwa miongoni mwa miradi itakayobadilisha kwa kiasi kikubwa
huduma za afya katika Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani mara
utakapokamilika.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila akizungumza.


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya na Meneja wa Mkataba wa mradi huo, Festo Mapunda, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto pamoja na Maabara ya Kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






















Post a Comment