" KATAMBI AWAHIMIZA VIONGOZI WA DINI KUILINDA AMANI YA TANZANIA

KATAMBI AWAHIMIZA VIONGOZI WA DINI KUILINDA AMANI YA TANZANIA



Na Mapuli Kitina Misalaba

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, amewataka viongozi wa dini nchini kuendelea kuhubiri amani, upendo na maadili mema ili kulinda umoja wa taifa, akieleza kuwa mmomonyoko wa maadili umekuwa tishio kubwa kwa ustawi wa Tanzania kuliko hata janga la UKIMWI.

Mhe. Katambi ameyasema hayo leo Juni 28 alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ibada ya uchangiaji wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Shinyanga.

Akizungumza mbele ya waumini na viongozi mbalimbali wa dini na serikali, Waziri Katabi amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ina jukumu la kuhakikisha usalama wa wananchi, kulinda amani na kusimamia utekelezaji wa sheria, lakini juhudi hizo haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa viongozi wa dini.

Ameeleza kuwa Tanzania imeanza kushuhudia dalili za kuporomoka kwa maadili ya jamii, hali ambayo inaweza kuhatarisha mshikamano na amani ya nchi ikiwa haitadhibitiwa mapema.

Waziri Katambi ameongeza kuwa baadhi ya watu wamekuwa tayari kuchochea vurugu na machafuko kwa ajili ya kupata madaraka au maslahi binafsi, hali inayotishia amani ambayo Tanzania imeijenga kwa miaka mingi.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imebaini uwepo wa kampeni mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii zinazowashawishi vijana kujiunga na vikundi vinavyohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani.

Amesema serikali pia imekuwa ikifuatilia na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaosambaza video na ujumbe unaochochea uharibifu wa shule, majengo ya serikali na miundombinu ya umma pamoja na kuhamasisha vitendo vya uhalifu.

Pamoja na hayo, Waziri Katambi amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira bora ya malezi kwa watoto na vijana ili kujenga kizazi chenye maadili, uzalendo na uwajibikaji.

Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria, Dkt. Yohana Nzeru, amesema kanisa linaendelea kuthamini ushirikiano uliopo kati yake na serikali katika kuwahudumia wananchi na kujenga jamii yenye maadili.

Ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kuongeza fursa za elimu bora kwa watoto wa Shinyanga na maeneo jirani, huku ukilenga kuwalea katika misingi ya elimu, maadili na hofu ya Mungu.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Patrobas Katambi





 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post