Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi, Juni 28, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Mtumba, jijini Dodoma
Na Meleka Kulwa – Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo imechangia ukuaji wa uchumi kufikia wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025, huku matarajio yakionyesha kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026.
Pia amesema hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita zimeiwezesha nchi kuongeza kiwango cha kujitegemea kifedha hadi asilimia 74.2, huku mapato ya ndani yakichangia sehemu kubwa ya bajeti ya taifa inayofikia shilingi trilioni 62.33.
Ameyasema hayo Juni 28, 2026, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo nchini.
“Ukuaji wa uchumi umeendelea kuimarika na kufikia wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025, huku matarajio yakionyesha kufikia asilimia 6.3 mwaka 2026, sambamba na kudhibiti mfumuko wa bei ambao umeendelea kubaki ndani ya kiwango cha asilimia 3.4,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta za nishati, maji, afya, elimu, usafirishaji na kilimo, ikiwemo miradi ya kimkakati kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, reli ya SGR, uboreshaji wa bandari na upanuzi wa mtandao wa umeme nchini.
Amebainisha kuwa kupitia uwekezaji huo, uzalishaji wa umeme umeongezeka hadi megawati zaidi ya 4,000, huku miradi mingine ikilenga kufikia zaidi ya megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Katika sekta ya kilimo, Msigwa amesema uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 38, hali iliyowezesha taifa kufikia asilimia 130 ya utoshelevu wa chakula.
“Serikali imeendelea kupanua huduma za maji mijini na vijijini, ambapo upatikanaji wa maji umeongezeka hadi asilimia 85 vijijini na zaidi ya asilimia 92 mijini,” amesema.
Aidha amebainisha Kuwa , miradi ya barabara, reli, viwanja vya ndege na usafirishaji wa majini imeboreshwa kwa kiasi kikubwa, hatua inayochochea ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya usimamizi thabiti wa Serikali na ushirikiano wa wananchi, akisema Tanzania inaendelea kujengwa na Watanzania wenyewe kupitia rasilimali na mipango ya ndani.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano, pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, akisema Serikali itaendelea kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi wote kwa usawa.
Post a Comment