" NYANDOLWA FC YAVUKA KIKWAZO CHA SHILABELA FC KWA PENATI , YATINGA ROBO FAINALI NIACHEKONA CUP 2026

NYANDOLWA FC YAVUKA KIKWAZO CHA SHILABELA FC KWA PENATI , YATINGA ROBO FAINALI NIACHEKONA CUP 2026


Na Mapuli Kitina Misalaba


Timu ya Nyandolwa FC imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa penati dhidi ya Shilabela FC katika mchezo uliochezwa leo Juni 10, 2026 kwenye Uwanja wa Mwabenda, Kata ya Solwa.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulimalizika kwa sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 za kawaida, hali iliyolazimu mshindi kupatikana kwa mikwaju ya penati kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo.

Katika hatua ya mikwaju ya penati, Nyandolwa FC ilionesha utulivu na umakini mkubwa kwa kufunga penati zake tatu za mwanzo, huku Shilabela FC ikikosa penati zote tatu za awali na hivyo kushindwa kuendelea na mashindano hayo.

Ushindi huo umeifanya Nyandolwa FC kufuzu rasmi hatua ya robo fainali huku safari ya Shilabela FC katika mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 ikifikia tamati.

Baada ya mchezo huo, viongozi wa Shilabela FC wameushukuru uongozi wa mashindano pamoja na mwandaaji kwa kuwapa nafasi ya kushiriki. Aidha, wameomba Kamati ya Mashindano kuzingatia uwezekano wa kurejeshwa kwa nafasi ya “Best Rooza” ili kutoa fursa kwa baadhi ya timu zilizoondolewa kuendelea kushiriki katika hatua za baadaye.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Katibu wa Kamati ya Mashindano ya NIACHEKONA CUP, Sambayi Jilya, ametangaza ratiba ya mchezo wa kesho ambapo Bulige FC itamenyana na Manheigana FC katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku kila timu ikisaka nafasi ya kutinga hatua inayofuata.

Sambayi Jilya amewahimiza wananchi, wadau wa michezo na mashabiki kuendelea kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Mwabenda kushuhudia michezo mbalimbali inayoendelea kuibua vipaji vya vijana na kuimarisha mshikamano wa jamii.

Mashindano ya NIACHEKONA CUP 2026 yameandaliwa na Bwana Paul Daud Augustino maarufu MC NIACHEKONA kwa ufadhili wa Shirika la Lushu Foundation, yakiwa na lengo la kuibua vipaji vya vijana, kukuza michezo, kuimarisha amani na mshikamano wa jamii.

Kwa mawasiliano ya shughuli mbalimbali za kijamii, michezo, matangazo na ushereheshaji wa matukio, wasiliana na MC NIACHEKONA kupitia namba 0757 267 738.

Kikosi cha Shilabela FC.




 

Post a Comment

Previous Post Next Post