Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesaini hati tatu za makubaliano ya ushirikiano wa kielimu na Urusi zitakazowezesha kubadilishana wataalamu, kuendeleza tafiti za pamoja na kuongeza fursa za elimu ya juu kwa wanafunzi wa nchi hizo mbili.
Akitoa taarifa hiyo kwa Waandishi wa Habari Juni 10, 2026 jijini Dodoma Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya ziara ya kihistoria nchini humo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imeleta mafanikio katika nyanja za elimu, sayansi na teknolojia
Waziri Mkenda ametaja makubaliano yaliyofanyika ya kwanza ni kati ya Wizara ya Elimu ya Tanzania na Wizara ya Elimu ya Urusi yanayolenga kubadilishana walimu na wataalamu, kuendesha semina za pamoja na kufundisha lugha za Kiswahili na Kirusi.
Makubaliano ya pili ambayo Wizara imeingia yamehusisha Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) na Chuo Kikuu cha RUDN, ambapo wanafunzi wa kitanzania watapata fursa ya kusoma shahada ya kwanza ya Teknolojia ya Anga kupitia mfumo wa shahada pacha, wakisoma miaka miwili Tanzania na miaka miwili nchini Urusi
“Kupitia programu hii, wanafunzi watatumia mtaala wenye viwango vya kimataifa, kusoma kwa lugha ya kingereza nchini Tanzania na kujifunza lugha ya Kirusi kabla ya kuendelea na masomo yao nchini Urusi. Hatua hii itaongeza uwezo wa taifa katika sayansi, teknolojia na uhandisi.” Amesema Waziri Mkenda
Hati ya tatu ya makubaliano kati ya DIT na Chuo Kikuu cha RUDN inalenga programu za shahada ya uzamili, ambapo wanafunzi watapata nafasi ya kusoma katika nchi zote mbili na kutunukiwa shahada zinazotambulika kimataifa, huku ushirikiano huo ukifungua milango mipya ya utafiti na ubunifu.
"Chuo Kikuu cha RUDN kimeahidi kutoa ufadhili wa masomo (scholarships) kumi kwa wanafunzi wa Kitanzania. Ufadhili huu, utawawezesha Watanzania kusoma nje ya nchi kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended DS/AI+" amesema Prof Mkenda.
Mafanikio haya yanafuatia ziara ya kihistoria ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi mapema mwezi huu yakilenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kielimu kati ya Tanzania na Urusi, huku akipata heshima ya kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima kutoka Chuo Kikuu cha RUDN, kutambua mchango wake katika uongozi na maendeleo ya kimataifa.
Post a Comment