Shirika la Kivulini
linaendelea kutekeleza mradi wa GROW ENRICH unaolenga kuboresha afya ya
mama na mtoto pamoja na kuongeza ushiriki wa wanaume katika masuala ya afya ya
familia. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la World Vision
Tanzania, ukiwa na lengo la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto
wachanga kupitia elimu, ushirikishwaji wa jamii na uimarishaji wa huduma za
afya.
Katika utekelezaji
wa mradi huo, Shirika la Kivulini limefanya midahalo ya kijamii katika Kata za
Mwalukwa na Usanda, zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Midahalo hiyo
iliwakutanisha wananchi, viongozi wa serikali, wataalamu wa afya na watumishi
wa Shirika la Kivulini ili kujadili changamoto zinazoikabili afya ya mama na
mtoto pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua.
Kata ya Mwalukwa: Jamii Yapata Elimu
na Kuweka Maazimio ya Mabadiliko
Mdahalo uliofanyika
Kata ya Mwalukwa ulifanikiwa kwa kiwango kikubwa ambapo wananchi walipata elimu
mbalimbali kuhusu afya ya uzazi, malezi na umuhimu wa ushiriki wa baba katika
afya ya familia.
Akizungumza katika
mdahalo huo, Meneja wa Mradi wa GROW ENRICH, Mageni Malulu, alisema kuwa mradi
huo unafanya kazi kwa karibu na vituo vya afya na zahanati kwa kuwajengea uwezo
watumishi wa afya pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuboresha huduma
zinazotolewa kwa mama na mtoto.
"Mradi huu
unalenga kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua. Pia tumekuwa
tukianzisha vikundi mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo vikundi vya Baba Bora,
vinavyowahamasisha wanaume kushiriki kikamilifu katika huduma za afya ya
familia na malezi ya watoto," alisema Malulu.
Aliongeza kuwa
vikundi hivyo vinaendelea kuwafikia wanaume wengi zaidi na kuwawezesha kuwa
sehemu ya maamuzi na huduma zinazohusu afya ya familia.
Polisi Jamii Watoa Elimu Dhidi ya
Ukatili wa Kijinsia
Katika mdahalo huo,
Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Polisi Jamii lilishiriki kutoa elimu kuhusu
kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Polisi walisisitiza
kuwa baba ana wajibu wa kuwa mlinzi wa familia yake kwa kuhakikisha anazuia
vitendo vya ukatili na kujenga mazingira salama kwa wanawake na watoto.
Aidha, Koplo
Gabriel alitumia sanaa ya uimbaji kuelimisha wananchi kuhusu madhara ya
ukatili wa kijinsia pamoja na umuhimu wa kuzingatia sheria na usalama
barabarani, jambo lililowavutia wananchi wengi na kufanya ujumbe kufika kwa
urahisi.
Bodaboda Wakabidhiwa Vizibao vya Elimu
Katika kuongeza wigo
wa kufikisha ujumbe kwa jamii, madereva wa bodaboda walikabidhiwa vizibao
vyenye ujumbe wa kuhamasisha ushiriki wa baba katika afya ya mama na mtoto.
Hatua hiyo inalenga
kuhakikisha ujumbe unaendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia bodaboda
ambao hukutana na watu wengi katika shughuli zao za kila siku.
Sababu Zinazochangia Ushiriki Mdogo wa
Baba
Mdahalo ulioongozwa
na Afisa Maendeleo wa Kata ya Mwalukwa, Elipendo John, uliwapa wananchi
nafasi ya kueleza changamoto zinazowafanya baadhi ya wanaume kushindwa
kushiriki kikamilifu katika afya ya mama na mtoto.
Baadhi ya sababu
zilizotajwa ni:
- Mila na desturi zinazotafsiri
huduma za afya ya uzazi kuwa ni jukumu la wanawake pekee.
- Ukosefu wa elimu kuhusu nafasi ya
baba katika afya ya familia.
- Majukumu ya kiuchumi na shughuli
za kutafuta kipato.
- Hofu au aibu ya kwenda kliniki
pamoja na wenza wao.
- Mawasiliano hafifu kati ya
wanandoa kuhusu masuala ya afya ya uzazi.
Baada ya mjadala
huo, wananchi waliweka maazimio ya pamoja yatakayofuatiliwa ili kuongeza
ushiriki wa wanaume katika afya ya familia.
Elimu ya Lishe Yaongeza Uelewa wa
Jamii
Afisa Lishe
aliyeshiriki mdahalo huo alitoa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa mama
mjamzito, mama anayenyonyesha na mtoto.
Alisisitiza kuwa
baba ana nafasi muhimu katika kuhakikisha familia inapata lishe bora kwa:
- Kushiriki kupanga na kununua
vyakula vyenye virutubisho.
- Kumsaidia mama wakati wa ujauzito
na kipindi cha kunyonyesha.
- Kuhamasisha mahudhurio ya kliniki
kwa mama na mtoto.
- Kushiriki malezi ya mtoto tangu
kuzaliwa.
- Kuweka mazingira yanayomwezesha
mama kupata mapumziko na huduma stahiki.
Michezo Yatumika Kufikisha Ujumbe wa
Afya
Shughuli hiyo
ilipambwa na burudani mbalimbali ikiwemo mashindano ya mpira wa miguu ambapo
wanaume wa kijiji waligawanywa katika timu za Simba na Yanga.
Mashindano hayo
yaliwavutia wananchi wengi kujitokeza kushuhudia mchezo huo. Wakati wa
mapumziko, wataalamu walitoa elimu kuhusu afya ya mama na mtoto pamoja na
umuhimu wa baba kushiriki katika malezi na afya ya familia. Baada ya mchezo
kuendelea na kumalizika, mdahalo uliendelea huku elimu ikiendelea kutolewa kwa
wananchi waliohudhuria.
Kata ya Usanda: Mashindano ya Baiskeli
Yavutia Wananchi
Utekelezaji wa
shughuli uliendelea katika Kata ya Usanda ambapo ulianza kwa mashindano ya
baiskeli yaliyowashirikisha wanaume kutoka katika jamii.
Mashindano hayo
yaliwavutia wananchi wengi kujitokeza, hali iliyotoa fursa nzuri ya kufikisha
ujumbe wa mradi kwa idadi kubwa ya watu.
Baada ya mashindano
hayo, mdahalo ulifanyika ukiongozwa na Afisa Maendeleo, Afisa Lishe, Mwenyekiti
wa Kijiji pamoja na maafisa kutoka Shirika la Kivulini.
Wananchi walipata
elimu kuhusu afya ya mama na mtoto, umuhimu wa ushiriki wa baba katika malezi
na huduma za afya, huku wakikubaliana kwa pamoja maazimio mbalimbali
yatakayosaidia kuongeza ushiriki wa wanaume katika afya ya familia.
Aidha, madereva wa
bodaboda katika kata hiyo walikabidhiwa vizibao vyenye ujumbe maalumu wa
kuhamasisha ushiriki wa baba katika malezi na afya ya mama na mtoto ili ujumbe
huo uendelee kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Wananchi Wanufaika
na Huduma za Afya Bure
Mbali na midahalo na
utoaji wa elimu, shughuli zote zilizofanyika katika Kata za Mwalukwa na Usanda
ziliambatana na utoaji wa huduma za afya bila malipo kwa wananchi. Huduma hizo
zilitolewa na wataalamu wa afya kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za
kinga na uchunguzi wa mapema wa magonjwa mbalimbali.
Wananchi walipata
fursa ya kupimwa Virusi vya UKIMWI (VVU), kiwango cha wingi wa damu
(Hemoglobin), magonjwa ya zinaa pamoja na vipimo vingine vya msingi vya
afya kulingana na mahitaji. Aidha, huduma za ushauri nasaha zilitolewa kwa
wananchi ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao, afya za wenza
wao na ustawi wa familia kwa ujumla.
Huduma hizo
zilihamasisha wananchi wengi kujitokeza kupima afya zao, kupata ushauri kutoka
kwa wataalamu na kuelewa umuhimu wa uchunguzi wa afya wa mara kwa mara. Kupitia
huduma hizi, Mradi wa GROW ENRICH umeendelea kuhamasisha jamii kuchukua hatua
za mapema katika kulinda afya ya mama, mtoto na familia kwa ujumla.
Kupitia Mradi wa
GROW ENRICH, Shirika la Kivulini linaendelea kushirikiana na serikali,
wataalamu wa afya na jamii kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaendelea
kuimarika huku likihamasisha wanaume kuwa washiriki muhimu katika malezi na
ustawi wa familia.
Kupitia midahalo, elimu, michezo na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, mradi huu unaendelea kujenga jamii yenye uelewa mkubwa zaidi kuhusu afya ya familia na kuchangia kupunguza vifo vya mama na mtoto katika Wilaya ya Shinyanga.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




































































































Post a Comment