" WAZIRI MKUU AHIMIZA WATANZANIA KUONGEZA USHIRIKI KATIKA KUWAHUDUMIA WAZEE

WAZIRI MKUU AHIMIZA WATANZANIA KUONGEZA USHIRIKI KATIKA KUWAHUDUMIA WAZEE



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema umefika wakati kwa Watanzania kuongeza ushiriki wao katika kuwahudumia makundi yenye uhitaji, hususan wazee, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi duniani yaliyopunguza utegemezi wa misaada ya wahisani na kuongeza wajibu wa jamii kushiriki katika utoaji wa huduma za kijamii.

Dkt. Mwigulu amesema hayo tarehe 29 Juni, 2026, alipokuwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Kuwaenzi Wazee na Harambee ya Kuchangia Ujenzi wa Kituo cha Wazee cha Petra (Petra Elderly Centre), iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Amesema Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya wazee kutokana na kuimarika kwa huduma za afya na kuongezeka kwa umri wa kuishi, hali inayohitaji Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuimarisha mifumo ya kuwahudumia wazee 

“Wazee wetu ni hazina ya hekima, busara, maarifa na historia ya Taifa. Tunapaswa kuendelea kuwaheshimu, kuwatunza na kutumia uzoefu wao katika kujenga kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Dkt. Mwigulu. 

Amesema pamoja na Serikali kuendelea kuboresha huduma kwa wazee kupitia sera, programu na bajeti mbalimbali, ushiriki wa wananchi, sekta binafsi, taasisi za dini na wadau wa maendeleo una nafasi kubwa katika kuhakikisha wazee wanaendelea kuishi kwa heshima, usalama na utu. 

Aidha, Waziri Mkuu amesema mabadiliko ya mifumo ya maisha yameifanya jamii kuhitaji mbinu mpya za kuwahudumia wazee, hivyo ameipongeza Petra Elderly Centre kwa kuanzisha mradi utakaowawezesha wazee kupata huduma za makazi, afya, ustawi wa kisaikolojia pamoja na fursa ya kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii na kuhamisha maarifa yao kwa vijana. 

“Hatujengi majengo pekee, tunajenga furaha ya Watanzania. Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zote zinazolenga kuboresha ustawi wa wananchi,” amesema Dkt. Mwigulu. Awali, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha ustawi wa wazee kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, Toleo la mwaka 2024, pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya ustawi wa jamii nchini. 

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha huduma katika vituo vya ustawi wa jamii, ikiwemo vinavyohudumia wazee na wasiojiweza, huku ikiendelea kupitia sheria mbalimbali ili kuimarisha ulinzi wa haki na ustawi wa wazee. 

Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Petra Elderly Centre, Dkt. Stergomena Tax, amesema kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuwawezesha wazee kuishi kwa utu, heshima na thamani, sambamba na kuendelea kutumia maarifa na uzoefu wao kwa manufaa ya jamii. 

Amesema ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi umefikia asilimia 24.5 na unahitaji takribani shilingi bilioni 3.6 ili kukamilika. Aliongeza kuwa kituo hicho kitatoa huduma za makazi, afya, tiba, ustawi wa kisaikolojia pamoja na programu za kuwaunganisha wazee na vijana kwa lengo la kuhifadhi na kurithisha maarifa, maadili na utamaduni wa Kitanzania. 

Naye Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Dar Es Salaam, Mzee Salum Matimbwa, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha sera zinazohusu wazee na kuomba kuharakishwa kwa mchakato wa kutungwa kwa sheria maalumu ya wazee ili kuimarisha zaidi ulinzi wa haki na ustawi wao.




Post a Comment

Previous Post Next Post