Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amewataka Waandishi wa Habari nchini kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa weledi, uzalendo na maadili ya taaluma, akisisitiza kuwa kalamu wanayoitumia ina nguvu kubwa ya kujenga au kubomoa taifa kupitia taarifa wanazozifikisha kwa umma.
Bw. Msigwa ametoa wito huo tarehe 08 Julai, 2026 alipotembelea banda la Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), akisema waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee katika kuhamasisha maendeleo ya taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia taarifa zenye ukweli, usahihi na maslahi mapana ya nchi.
Alisema waandishi wa habari wa zamani walifundishwa kuwa kalamu ni chombo chenye nguvu kubwa kuliko silaha kwa sababu inaweza kuathiri fikra, maamuzi na mwelekeo wa jamii.
“Kwa sisi tuliosoma habari zamani tunajua kuwa kalamu ni hatari kuliko bunduki. Kalamu inaweza kuua kundi kubwa la watu, huku risasi ikiua kulingana na idadi ya risasi zake,” alisema Msigwa.
Aidha, aliwataka Waandishi wa Habari kujiepusha na kile alichokiita habari za kikasuku zinazorudia simulizi bila uchambuzi wa kina wala uhakiki wa taarifa, akisema mwenendo huo unadhoofisha taaluma ya habari na hauchangii maendeleo ya nchi.
“Tuepuke habari za kikasuku na waandishi wanaobagaza nchi yao. Tuwe na waandishi wanaosikiliza, wanaochambua na kueneza mema ya nchi yao ili kukuza uchumi,” alisisitiza Msigwa.
Msigwa alitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) kwa hatua kubwa iliyofikia katika kusajili, kuthibitisha na kutoa vitambulisho vya ithibati kwa Waandishi wa Habari nchini.
Alisema taarifa ambazo Wizara imekuwa ikipokea zinaonesha kuwa utekelezaji wa jukumu hilo umepokelewa vizuri na wadau wa sekta ya habari, huku Waandishi wa Habari wengi wakionesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa na Bodi huku akiwasisitiza waandishi wa Habari ambao bado hawajajisajili kuhakikisha wanapata ithibati kwa kuwa ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema hadi sasa zaidi ya Waandishi wa Habari 4,500 wamejisajili katika mfumo wa Bodi, ambapo kati yao zaidi ya 3,650 tayari wamepatiwa ithibati na vitambulisho vinavyowawezesha kutekeleza shughuli zao kwa mujibu wa sheria.
Post a Comment