
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), ametoa maagizo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), mkandarasi na wadau wote wanaotekeleza awamu ya pili ya mradi wa Umeme wa Jua uliopo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga kuhakikisha mradi huo unasimamiwa kwa ukaribu na kukamilika ndani ya muda wa miezi 17 uliopangwa, ili kuendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Maagizo hayo ameyatoa leo Julai 27, 2026, mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 204.7 kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni za Sagemcom Energy & Telecom SAS pamoja na STEG International Services kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 100 katika eneo la Ngunga, Wilaya ya Kishapu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Ndejembi amesema TANESCO ina wajibu wa kuhakikisha kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo inafuatiliwa kwa karibu ili kazi ifanyike kwa ubora unaotakiwa na kukamilika kwa wakati, akisisitiza kuwa mradi huo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kupitia vyanzo vya nishati jadidifu.
Aidha, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuzingatia kikamilifu masharti yote ya mkataba, ikiwemo ratiba ya utekelezaji wa kazi, viwango vya ubora wa ujenzi, usalama mahali pa kazi pamoja na ulinzi wa mazingira, akieleza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaoathiri utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
Vilevile, Waziri huyo ameitaka TANESCO kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi ili washiriki kikamilifu katika kuulinda, akisema ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha miundombinu ya maendeleo inalindwa dhidi ya vitendo vya uharibifu.
Katika kuhakikisha manufaa ya mradi yanawanufaisha wananchi wa eneo husika, Waziri Ndejembi pia amesisitiza kuwa mkandarasi ahakikishe stahiki zote za wafanyakazi wazawa zinazingatiwa kwa mujibu wa sheria, huku TANESCO ikiendelea kutoa kipaumbele kwa wahandisi na wataalamu wazawa kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Mbali na hilo, Waziri huyo ameitaka TANESCO kuongeza mchango wake katika maendeleo ya jamii kupitia programu za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kwa kujenga madarasa matano mapya katika eneo la mradi, tofauti na madarasa matatu yaliyojengwa wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza.
Akizungumzia mradi huo, Waziri Ndejembi amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika mseto wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme (Energy Mix), ambapo Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wa umeme wa gharama nafuu na unaotokana na nishati jadidifu.
Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili zenye uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 150. Awamu ya kwanza yenye uwezo wa Megawati 50 iligharimu Shilingi bilioni 118.3 na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji, huku awamu ya pili yenye uwezo wa Megawati 100 ikigharimu Shilingi bilioni 204.7, hivyo kufanya gharama za jumla za mradi kufikia Shilingi bilioni 323.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kukamilika kwa mradi huo kutachangia kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vya nishati jadidifu, kuimarisha uthabiti wa mfumo wa umeme nchini na kusaidia Serikali kufikia lengo la kuwa na umeme wa kutosha kwa matumizi ya sasa na ya baadaye.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Wizara ya Nishati na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga watausimamia mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ubora na kukamilika kama ilivyopangwa.
Amesema mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa awamu ya kwanza yanatoa matumaini kuwa awamu ya pili pia itatekelezwa kwa ufanisi mkubwa, huku akisisitiza kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, ameahidi kuwa shirika hilo litamsimamia mkandarasi kwa karibu katika kila hatua ya utekelezaji ili kuhakikisha kazi zote zinafanyika kwa ubora unaotakiwa na mradi unakamilika ndani ya muda uliokubaliwa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mkandarasi, Joao Jirio, amesema kampuni hiyo ipo tayari kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia masharti yote ya mkataba na kuhakikisha unakamilika kwa wakati, huku ukifikia viwango vya kimataifa vya ubora.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi na wadau wa sekta ya nishati.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






























Post a Comment