" SHINYANGA YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU KUPITIA ELIMU YA UHAMIAJI SALAMA

SHINYANGA YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU KUPITIA ELIMU YA UHAMIAJI SALAMA


Na Mapuli Kitina Misalaba

Jitihada za kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu zimeendelea kuimarishwa mkoani Shinyanga kupitia utoaji wa elimu kuhusu uhamiaji salama, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulinda haki za wanawake, watoto, vijana na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.

Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa, Rehema Edson, wakati wa semina ya mafunzo kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu na uhamiaji salama kwa maafisa wa serikali.

Edson amesema usafirishaji haramu wa binadamu ni moja ya changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuzuia wananchi, hususan wasichana na wanawake, kutumbukia katika mikono ya wahalifu wanaotumia ahadi za ajira na maisha bora kuwashawishi.

Amesema elimu ya uhamiaji salama ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi wanapotafuta ajira au fursa za maisha, hivyo kupunguza uwezekano wa kudanganywa na kusafirishwa kinyume cha sheria.

Kwa upande wake, mwezeshaji kutoka Shirika la CVM, Mwajuma Ally, amesema mradi unaotekelezwa unalenga kuwainua wafanyakazi wa majumbani, hasa wasichana, kwa kuwapa maarifa kuhusu haki zao pamoja na kuwaunganisha na fursa za mafunzo na ajira zenye staha.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, wafanyakazi wa majumbani wanawezeshwa kupata elimu kuhusu haki zao, mafunzo ya ujuzi kupitia VETA, ajira zenye staha pamoja na elimu ya uhamiaji salama ili kupunguza uwezekano wa kudhurumiwa au kuingia katika mazingira ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Mafunzo hayo yamewakutanisha maafisa wa serikali na wadau mbalimbali kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu namna ya kutambua viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu, kuimarisha ulinzi wa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi na kuongeza ushirikiano katika kuzuia uhalifu huo.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post