NA: DK. REUBENI LUMBAGALA Kuna umuhimu mkubwa kwa Watanzania kubadili mtizamo kuhusiana na lugha ya Kiswahili. Hii ina maana kuwa, tusiiangalie lugha ya Kiswahili katika muktadha wa mawasiliano pekee. Hapana. Ni kwamba, twende mbele zaidi, yaani tukifanye Kiswahili kuwa bidhaa ya kuuza na kuingiza fedha, kuongeza ajira, hatimaye kukuza uchumi na maendeleo ya mama Tanzania badala ya Kiswahili kubaki kama chombo cha mawasiliano na kupiga soga.Kiswahili kimepiga hatua kubwa sana na kupata heshima kubwa ulimwenguni. Tuna kila sababu ya kujivunia lugha hii adhimu na adimu, ambayo tunapaswa kuifungamanisha na mikakati ya ukuzaji uchumi kwa maendeleo endelevu.Ni hivi: Lugha ya Kiswahili imevuka mipaka. Kwa sasa, Kiswahili si lugha ya Tanzania au Afrika Mashariki pekee bali ni lugha ya Afrika na ya dunia. Kiswahili sasa kimepata heshima kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). UNESCO imeichagua Julai 7, ya kila mwaka, kuwa "Siku ya Kiswahili Duniani".Na kwa mwaka huu, maadhimisho hayo, yanafanyika Jijini Paris, nchini Ufaransa, yalipo makao makuu ya UNESCO, ambapo Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amehudhuria maadhimisho hayo, kumuwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.Kwa hakika, kuna mwamko mkubwa wa watu kujifunza Kiswahili ulimwenguni. Aidha, Kiswahili sasa kinafundishwa katika shule na vyuo mbalimbali ulimwenguni, jambo linaloendelea kuongeza thamani yake. Kukibidhaisha Kiswahili kunahusisha kuingiza fedha kupitia lugha hiyo. Sasa, tunawezaje kutengeneza fedha kupitia lugha ya Kiswahili?Kwanza, kupitia ajira ya kufundisha Kiswahili. Wapo vijana wengi wahitimu wa vyuo na vyuo vikuu waliosomea somo la Kiswahili. Hawa wanaweza kutumika kufundisha Kiswahili kwa wageni wanaopenda kujifunza lugha hii.Aidha, kupitia shughuli hiyo, vijana hao wataingiza fedha na serikali kunufaika kupitia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wake na kupata kodi kupitia mishahara ya walimu hao, jambo litakalochangia katika kukuza uchumi.Pili, kuuza matini za Kiswahili. Wataalamu wa Kiswahili wanaweza kuingiza fedha kupitia kuandika na kuuza vitabu vya Kiswahili vilivyo katika muundo wa nakala laini na nakala ngumu (soft and hard copies). Mauzo hayo, yatawezesha kujenga uchumi wa nchi yetu na kukuza maendeleo.Tatu, kukifungamanisha Kiswahili na sanaa ya filamu na tamthiliya za nje. Serikali ishirikiane na wandaaji wa filamu na tamthiliya za nje kama Korea, Uturuki, India na wengineo katika kutafsiri filamu na tamthiliya hizo kwa kutumia Kiswahili. Hii itaongeza fursa za ajira kwa 'waingizaji wa sauti za Kiswahili' katika tamthiliya hizo na hivyo kuwezesha wahusika hao kupata kipato. Jambo hili natamani liendelee kufanyika kwa ukubwa zaidi ya linavyofanyika sasa.Jambo muhimu, ni wataalamu wetu wa Kiswahili kuwa na umahiri katika lugha nyingine za kimataifa kama Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kijerumani, Kiarabu, Kikorea, kutaja kwa uchache ili waweze kuwa walimu mahiri wa kufundisha wanafunzi wa kigeni na kuongeza mawanda ya kupata fursa za kufundisha lugha hiyo ulimwenguni.Kimsingi, hata safari ya miaka 25 ijayo, kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, Kiswahili kina nafasi ya kuchangia kufanikisha mipango mingi ya kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo katika kukibidhaisha kama nilivyoeleza katika nyanja ya uchumi.Mungu Ibariki Tanzania.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment