Na Mwandishi Wetu, Chalinze
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema utekelezaji wa hatua za mwisho za Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma utasababisha kukosekana kwa huduma ya umeme kwa muda katika baadhi ya mikoa, ili kupisha kazi za mkandarasi kwa kuzingatia usalama.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowele, amesema mradi huo umefikia asilimia 94 na unatarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026. Amesema hatua iliyobaki ni kuvuta nyaya katika maeneo ya Mkambalani, Morogoro na Kikombo, Dodoma, kazi inayohitaji kuzimwa kwa baadhi ya njia za kusafirisha umeme.
Amesema kazi hiyo itafanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itaanza Julai 30 hadi Agosti 4, 2026 katika eneo la Mkambalani, Morogoro, huku awamu ya pili ikifanyika Agosti 11 hadi 17, 2026 katika eneo la Kikombo, Dodoma.
Gowele amesema huduma ya umeme inaweza kukosekana kati ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni katika siku na maeneo tofauti, akisisitiza kuwa si wateja wote watakosa umeme kwa siku zote za kipindi hicho. Ratiba za maeneo yatakayoathirika zitatolewa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na makundi rasmi ya WhatsApp ya TANESCO.
Amefafanua kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara haitaathirika na zoezi hilo, huku mikoa mingine katika kanda ya kati, kaskazini, ziwa, magharibi na kusini magharibi ikitarajiwa kuathirika kwa nyakati tofauti.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma wenye urefu wa kilomita 345, Mhandisi Newton Mwakifamba, amesema mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 514 umefadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha usafirishaji wa umeme wote unaozalishwa katika Bwawa la Julius Nyerere wenye uwezo wa megawati 2,115, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini na kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika biashara ya umeme kupitia mifumo ya East African Power Pool na Southern African Power Pool.
TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
Post a Comment