" WACHIMBAJI WADOGO KAHAMA WALILIA UMEME NA MAJI, WASEMA HUDUMA ZITAKUZA UCHUMI NA AJIRA

WACHIMBAJI WADOGO KAHAMA WALILIA UMEME NA MAJI, WASEMA HUDUMA ZITAKUZA UCHUMI NA AJIRA

Na Paul Kayanda, KahamaWachimbaji wadogo wa dhahabu katika kijiji cha Bukooba, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wameiomba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwafikishia huduma za umeme na maji, wakisema miundombinu hiyo ni nguzo muhimu ya kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uendeshaji wa migodi na kuimarisha ajira kwa vijana.Ombi hilo limetolewa mbele ya waandishi wa habari waliotembelea mgodi huo kujionea shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, ambapo wachimbaji walieleza kuwa pamoja na mchango wao katika kukuza uchumi wa taifa, bado wanakabiliwa na changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta hiyo.Mkurugenzi Mkuu wa mgodi huo, Said Ibrahim Kapesya, alisema ukosefu wa umeme wa uhakika unawalazimu kutumia dizeli na petroli kuendesha mitambo ya uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu, hali inayoongeza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji kutokana na kupanda kwa bei za mafuta.Alisema endapo umeme wa gridi ungefika katika eneo hilo, gharama za uzalishaji zingepungua, uzalishaji ungeongezeka na wachimbaji wengi zaidi wangeweza kuwekeza katika teknolojia za kisasa za uchimbaji."Kwenye mgodi wetu changamoto kubwa ni ukosefu wa umeme wa kuendeshea mitambo. Tunatumia dizeli na petroli ambazo gharama zake ni kubwa sana. Tunaamini tukipata umeme tutafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuongeza uzalishaji," alisema Kapesya.Mbali na umeme, alisema mgodi huo pia unakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji kwa ajili ya shughuli za uchenjuaji wa dhahabu, jambo linalowalazimu kuyafuata maji kutoka maeneo ya mbali na kuongeza gharama pamoja na kuchelewesha uzalishaji."Tunaiomba Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kutusogezea huduma ya maji. Kwa sasa tunatumia fedha nyingi kusafirisha maji kutoka mbali, jambo ambalo linaathiri shughuli zetu za kila siku," alisema.Kapesya aliishukuru Serikali kwa kuwapatia leseni za utafiti na uchimbaji wa madini, akisema hatua hiyo imewapa fursa Watanzania wengi kuingia katika shughuli za uchimbaji na kujiongezea kipato.Hata hivyo, alimuomba Waziri wa Madini kuendelea kuwapa nafasi wachimbaji wadogo wanaokabiliwa na changamoto za kifedha badala ya kufuta leseni zao kwa haraka, akieleza kuwa wengi wao wanahitaji muda wa kujiimarisha kiuchumi ili kuendeleza shughuli zao.Alisema migodi ya wachimbaji wadogo ina mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana na wanawake, huku akibainisha kuwa mgodi wa Bukooba pekee umewezesha zaidi ya Watanzania 500 kujiajiri kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na uchimbaji wa madini."Leseni yetu imezalisha ajira kwa zaidi ya watu 500, wengi wao ni vijana na wanawake. Hii inaonyesha kuwa sekta ya uchimbaji mdogo ni muhimu katika kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla," alisema.Aidha, aliitaka Serikali kushirikiana na taasisi za fedha kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kununua vifaa vya kisasa vya utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.Alisema upatikanaji wa mitaji na teknolojia bora utasaidia kuongeza tija, kuboresha usalama migodini na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za madini.Wachimbaji hao wana matumaini kuwa utekelezaji wa miradi ya umeme na maji katika eneo lao utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya sekta ya uchimbaji mdogo, kuongeza uzalishaji wa dhahabu na kuifanya Kahama kuendelea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yanayochangia ukuaji wa sekta ya madini nchini.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post