" WAFANYABIASHARA SOKO LA MALUNGA, KAHAMA, WATAKIWA KUJENGA VIBANDA KUEPUSHA UHALIFU, DIWANI AHMED ASISITIZA MAENDELEO NA USALAMA

WAFANYABIASHARA SOKO LA MALUNGA, KAHAMA, WATAKIWA KUJENGA VIBANDA KUEPUSHA UHALIFU, DIWANI AHMED ASISITIZA MAENDELEO NA USALAMA









Na Neema Nkumbi, Kahama




Diwani wa Kata ya Malunga, Ahmed Haruna, amewataka wafanyabiashara wanaomiliki vibanda kwenye soko la Malunga Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, kukamilisha ujenzi wa vibanda wanavyomiliki ndani ya miezi mitatu.




Haruna amesema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaoshindwa kutekeleza hatua hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu.




Uamuzi huo umefikiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika ndani ya soko hilo, ukiongozwa na Diwani huyo pamoja na Mtendaji wa Kata ya Malunga, Rogath Kimario.




Uamuzi huo unafuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa vibanda kwa zaidi ya miaka 13, hali inayodaiwa kuchangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na kudumaa kwa biashara katika soko hilo.





Akizungumza katika mkutano huo, Haruna ametaja vipaumbele vyake baada ya kuchaguliwa kuwa ni pamoja na kuboresha Soko la Malunga ili liendane na hadhi ya masoko mengine yaliyopo ndani ya Manispaa.




"Tulipoanza kazi niliona kuna mambo mengi hayako sawa. Tukishirikiana na wananchi wa Malunga kuyarekebisha kata yetu itang'ara zaidi ya ilivyo sasa na moja ya maeneo yanayohitaji mabadiliko ni soko hili. amesema Haruna




Amesema baada ya kufuatilia nyaraka, serikali ilibaini kuwa asilimia kubwa ya vibanda vilivyotolewa tangu mwaka 2013 vinamilikiwa na wananchi wa Kata ya Malunga, lakini wengi wao hawajakamilisha ujenzi licha ya kupewa maeneo hayo kwa lengo la kuendeleza soko.




"Tulipofuatilia nyaraka, tukabaini waliogawiwa vibanda ni wananchi wa Malunga. Tunawaomba kila mwenye kibanda na kila mwenye meza ajenge eneo lake ili soko hili libadilike liwe na hadhi ya masoko ya Manispaa.




Haruna amesema baada ya mashauriano yaliyowashirikisha viongozi wa serikali ya mtaa, watendaji na viongozi wengine wa kata, imekubaliwa kutoa muda wa mwisho wa miezi mitatu kwa wamiliki wote kujitokeza kuthibitisha umiliki na kukamilisha ujenzi wa vibanda vyao.




Amesisitiza "Kuanzia Agosti mosi tunaanza kuhesabu miezi mitatu. Baada ya muda huo kuisha Serikali itaingia kwenye hatua ya utekelezaji, Hatutaki baadaye mtu aseme hakujulishwa."




Aidha, amewataka wamiliki wa vibanda kufika kwa viongozi wa serikali ya mtaa kujaza nyaraka za uthibitisho wa umiliki ili kurahisisha utekelezaji wa maamuzi yatakayochukuliwa baada ya Novemba 30, 2026.




Amesema kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo kutasaidia kuimarisha usalama, kuongeza ajira kwa wananchi, kukuza biashara na kuongeza mapato ya Halmashauri.




Wananchi waliohudhuria mkutano huo wameunga mkono uamuzi huo, wakisema vibanda na maboma ambayo hayajakamilika yamegeuka maficho ya wahalifu na chanzo cha hofu kwa wananchi, hususani nyakati za usiku.




Mkazi wa Malunga, Boniveture Maganga, amesema hali hiyo imekuwa ikihatarisha usalama wa wananchi na wafanyabiashara wanaopita eneo hilo.





Naye William Mond, Kamanda Mkuu wa Kata, amesema maboma na vichaka vilivyopo ndani ya soko hilo vimechangia kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu, hivyo kukamilika kwa ujenzi kutarejesha usalama na kufanya eneo hilo litumike kwa shughuli halali za biashara.





Bi. Sesilia Clement, Afisa Mtendaji Mstaafu wa Kata ya Malunga, amesema inasikitisha kuona mradi wa soko aliouanzisha ukiwa bado haujakamilika baada ya zaidi ya miaka 13, wakati kata nyingine zilizoanzishwa baadaye zimefanikiwa kuwa na masoko yanayofanya kazi kikamilifu.




"Inasikitisha kuona mradi huu umekwama kwa muda mrefu kiasi hiki Kata nyingi mpya zimeendelea, lakini Malunga imeendelea kubaki nyuma kutokana na kutokukamilika kwa soko hili," amesema.




Kwa upande wao wananchi waliohudhuria mkutano huo, wamependekeza wamiliki watakaoshindwa kukamilisha vibanda vyao ndani ya muda uliotolewa wavuliwe umiliki au wauze maeneo hayo kwa watu wenye uwezo wa kuyaendeleza, ili soko lianze kufanya kazi kikamilifu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kata ya Malunga.




















































Post a Comment

Previous Post Next Post