" Duni: Maridhiano yamefungua ukurasa mpya Zanzibar

Duni: Maridhiano yamefungua ukurasa mpya Zanzibar



MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji amesema mazungumzo yaliyozaa makubaliano yaliyofikiwa na kusainiwa yameandika historia mpya na kufungua ukurasa mpya kwa Zanzibar.

Duni alisema hayo kwenye mkutano wa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman alipozungumza na viongozi wa chama hicho kwa ngazi ya mkoa Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja jana.

Alisema viongozi wameahidi hadharani kwamba maafikiano hayo yatatekelezwa hatua kwa hatua.

“Niwatake Wazanzibari kushikamana ili kutetea mambo yote yaliyomo kwenye maridhiano, kwa kuwa yana manufaa kwa nchi na wala si viongozi na kuachana na habari zinazosambazwa zisizotutakia mema,” alisema.

Alisisitiza kwamba katiba bora na inayosimamiwa kwa umakini na uadilifu pamoja na kuondokana na utaratibu uliozoeleka hivi sasa wa kuwalinda watawala, itafanya mfumo huo kuwa madhubuti na kuheshimika kutokana na uwajibikaji uliotukuka.

Kwa upande wake, Othman alieleza na kufafanua maeneo yaliyomo katika makubaliano yaliyofikiwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na chama hicho na kusainiwa Julai 9, mwaka huu.

Alifafanua kuwa katiba ina nguvu iwapo viongozi wataisimamia na kuifuata vyema. Alisema kwa sasa imempa rais mamlaka makubwa kwa kuwa ndiye anayefanya kila kitu katika michakato mingi.

Akitaja baadhi ya mambo, alisema rais ndiye anayechagua mawaziri, majaji, kadhi mkuu, mwenyekiti wa tume na makamishna wake.

Post a Comment

Previous Post Next Post