Mwenyekiti
wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) Mkoa wa Shinyanga, Hatibu Madata
Mgeja, amewahimiza wahitimu kutumia kipindi cha mapumziko baada ya kumaliza
mitihani yao kujifunza ujuzi mbalimbali wa maisha, ikiwemo ufugaji, akisisitiza
kuwa dunia ya sasa haihitaji vyeti vya darasani pekee.
Mgeja ametoa
kauli hiyo Agosti 27, 2026, akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya 19 ya Kidato
cha Nne ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga, na kwamba amewasisitiza wahitimu
kujituma, kuwa na nidhamu, utiifu na kuendelea kutafuta maarifa nje ya yale
waliyofundishwa darasani.
Amesema
baada ya kumaliza mitihani yao, vijana watakuwa na kipindi cha mapumziko
ambacho wanapaswa kukitumia kujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji na
kujenga ujuzi ambao unaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye.
“Hivi
karibuni mtaenda kufanya mitihani yenu ya mwisho, baada ya mtihani mtakuwa na
mapumziko ya miezi kadhaa. Tumieni kipindi hicho kutafuta maarifa nje ya yale
mliyofundishwa shuleni, jifunzeni ufugaji wa kuku na ng’ombe. Mimi ni mfugaji,
nitawakaribisha shambani kwangu mje mjifunze,” amesema Mgeja.
Mgeja
amesema dunia ya sasa ina fursa nyingi ambazo zinaweza kuwawezesha vijana
kujenga maisha yao hata pale wanaposhindwa kuendelea na masomo, hivyo amewaasa
wahitimu kuwa wabunifu na kutumia fursa zinazowazunguka.
Mgeja pia
amewataka wahitimu hao kuwa mabalozi wa amani, uzalendo na kuipenda nchi yao,
huku akiwaasa kujiepusha na watu wanaopenda vurugu na fujo.
Amesema
Tanzania ni moja na hivyo vijana wana wajibu wa kulinda amani, umoja na
mshikamano wa taifa, akiwataka kutumia elimu na maarifa yao kwa manufaa ya
jamii.
Katika
mahafali hayo, Mgeja ameupongeza uongozi wa shule, walimu na wafanyakazi wasio
walimu kwa juhudi wanazofanya katika kusimamia taaluma na maadili ya wanafunzi.
Pia
amewapongeza wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga kwa kutoa
ushirikiano katika kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji muhimu wanapokuwa
shuleni, hususan chakula.
Mgeja ametoa
ahadi mbalimbali kwa shule hiyo, ikiwemo kutoa seti za jezi za mpira, pamoja na
tanki la maji, huku pia akiahidi kuchangia shilingi 600,000 katika ujenzi wa
miundombinu ya shule.
Kwa upande
wake, kaimu Afisa Elimu sekondari Manispaa ya Shinyanga Beatrice Senzighe Mbonea amewataka wahitimu kutumia
elimu waliyoipata shuleni kama msingi wa kuendelea kujifunza na kujenga maisha
yao.
Mbonea amesisitiza umuhimu wa kuwa na nidhamu, kujituma, kuheshimu wazazi na walezi pamoja na kutumia maarifa waliyojifunza kwa manufaa yao binafsi na jamii kwa ujumla.
Akizungumza
katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Old Shinyanga, Marco Msangwa
Itenga, amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo
ukosefu wa kisima cha maji, uzio wa shule kwa ajili ya kuimarisha usalama na
usimamizi wa nidhamu ya wanafunzi, matanki ya kuhifadhia maji pamoja na
upungufu wa nyumba za walimu.
Amesema
shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,282, wakiwemo wavulana 884 na wasichana
408, huku ikiwa na jumla ya walimu 34.
Katika
matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2025, shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 130
waliopata madaraja mbalimbali, ambapo wanafunzi 9 walipata Daraja la Kwanza, 16
Daraja la Pili, 52 Daraja la Tatu na 53 Daraja la Nne.
Itenga
amesema ni matumaini ya uongozi wa shule kwamba wanafunzi wanaotarajia kufanya
mtihani wao wa mwisho wa Kidato cha Nne mwezi Novemba 2026 watafanya vizuri
zaidi.
Amesema
shule hiyo pia imeendelea kufanya vizuri katika taaluma, ikiwemo kushika nafasi
ya kwanza kati ya shule 16 katika mtihani wa Mock Kanda uliofanyika Novemba
2025.
Katika
risala yake, Mkuu wa Shule ametoa shukrani kwa Serikali kupitia Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa fedha zilizotolewa kwa
ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule.
Ametaja
shilingi milioni 342.9 zilizotolewa mwaka 2025 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya
Awali na Msingi Butulwa, shilingi milioni 25 kwa ajili ya ukarabati wa vyumba
viwili vya madarasa, pamoja na shilingi milioni 31 zilizotolewa kwa ajili ya
ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa, jengo la utawala, viunga vya shule na
jengo la maabara.
Mahafali hayo ya 19 yamewakutanisha viongozi, walimu, wazazi, walezi na wanafunzi, huku Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akiwahimiza wahitimu kuendelea kuthamini elimu, kujenga nidhamu na kutumia maarifa na fursa zilizopo katika jamii kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akizungumza wakati wa Mahafali ya 19 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga, akiwahimiza wahitimu kutumia muda wao kujifunza ujuzi mbalimbali wa maisha.
Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akiwa katika picha ya pamoja.
Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa Kidato cha Nne katika Mahafali ya 19 ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga.
Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akizungumza wakati wa Mahafali ya 19 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga, akiwahimiza wahitimu kutumia muda wao kujifunza ujuzi mbalimbali wa maisha.
Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa Kidato cha Nne katika Mahafali ya 19 ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga.
Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akizungumza wakati wa Mahafali ya 19 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga, akiwahimiza wahitimu kutumia muda wao kujifunza ujuzi mbalimbali wa maisha.

Mgeni Rasmi, Hatibu Madata Mgeja, akizungumza wakati wa Mahafali ya 19 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga, akiwahimiza wahitimu kutumia muda wao kujifunza ujuzi mbalimbali wa maisha.
Awali Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 19 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Old Shinyanga, Hatibu Madata Mgeja, akiwasili katika eneo la shule kwa ajili ya kushiriki mahafali hayo.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






















Post a Comment