" FCC YAIMARISHA ELIMU YA USHINDANI NA ULINZI WA WALAJI

FCC YAIMARISHA ELIMU YA USHINDANI NA ULINZI WA WALAJI

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, ameshiriki kilele cha Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane, yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt.John Malecela Nzunguni Jijini Dodoma yakilenga kuimarisha tija, uzalishaji na upatikanaji wa masoko kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wa sekta ya kilimo nchini.

Maonesho hayo yaliyoongozwa na kaulimbiu “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya 2050”, yamefungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku yakitoa fursa kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali kuonesha huduma, bidhaa na fursa zinazolenga kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo.

Akizungumza mara baada ya kushiriki kilele hicho, Bi. Ngasongwa amesema ushiriki wa FCC katika maonesho hayo ulikuwa sehemu ya jitihada za kuifikisha elimu ya ushindani kwa wananchi, wazalishaji na wafanyabiashara ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa ushindani wa haki katika shughuli za kiuchumi.

Amesema FCC imeendelea kutumia majukwaa mbalimbali kama Nane Nane kutoa elimu kuhusu madhara ya bidhaa bandia na umuhimu wa wananchi kuwa makini wakati wa kununua bidhaa, kwa kuwa matumizi ya bidhaa zisizo halisi yanaweza kuathiri usalama wa watumiaji, ubora wa uzalishaji na ushindani wa biashara.

Bi.Ngasongwa amesisitiza kuwa elimu kwa wananchi ni muhimu katika kujenga soko lenye ushindani wa haki, ambapo wazalishaji na wafanyabiashara wanapata mazingira bora ya kushindana huku watumiaji wakilindwa dhidi ya vitendo vinavyoweza kuathiri maslahi yao.

Amesema FCC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha uelewa wa sheria za ushindani na ulinzi wa mlaji.

Ushiriki wa FCC katika Maonesho ya Nane Nane unaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga uchumi shindani na wenye tija, kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu na uelewa unaowawezesha kufanya maamuzi sahihi katika soko, huku wafanyabiashara wakihimizwa kuzingatia sheria, ubora wa bidhaa na ushindani wa haki.

Post a Comment

Previous Post Next Post