NA DENIS MLOWE, IRINGA 

MKUU wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta imezindua rasmi maandalizi ya maadhimisho ya jubilee ya miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga, huku ikitoa wito kwa wanafunzi wa zamani, wadau wa elimu, taasisi, kampuni na Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika kuifanya historia hiyo kuwa ya mafanikio.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamini Sitta, alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1926 imekuwa nguzo muhimu ya elimu bora, maadili na uongozi nchini, hivyo maadhimisho ya miaka 100 yanapaswa kuwa fursa ya kuenzi mchango wake kwa taifa.

Alisema maadhimisho hayo yatafanyika chini ya kauli mbiu isemayo, “Miaka 100 ya Elimu Bora, Maadili, na Uongozi wa Kuigwa,” kauli inayobeba historia ya shule hiyo katika kuzalisha viongozi, wataalamu na wazalendo waliolitumikia taifa kwa uadilifu na weledi.

Sitta alisema ratiba ya maadhimisho imeanza kupangwa ambapo Oktoba 8, 2026 kutafanyika matembezi ya Jubilee Walk pamoja na zoezi la usafi wa mazingira kwa lengo la kuhamasisha afya, uzalendo na utunzaji wa mazingira.

Alisema Oktoba 9 kutafanyika mbio za burudani (Fun Run) zitakazowakutanisha wanafunzi wa zamani wa Tosamaganga, wanafunzi wa sasa, wananchi na wadau mbalimbali, huku kilele cha maadhimisho kikitarajiwa kufanyika Oktoba 10, 2026.

Aliongeza kuwa siku ya kilele itahusisha maonyesho ya historia ya shule, nyaraka na kumbukumbu muhimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, utoaji wa tuzo za heshima pamoja na shughuli mbalimbali zitakazoonesha urithi mkubwa wa taasisi hiyo.

Alisema maadhimisho hayo hayatakuwa ya kusherehekea historia pekee, bali yataacha alama kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo kuboresha miundombinu ya shule, ununuzi wa basi la wanafunzi na miradi mingine itakayokubaliwa na wadau.

“Huu ni wakati wa wanafunzi wote wa zamani, marafiki wa Tosamaganga na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu na hata waliopo nje ya nchi tunawakaribisha kuungana nasi kuandika historia nyingine ya shule hii ya kipekee,” alisema Sitta.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mkoa wa Iringa inaamini maadhimisho hayo yatachochea uchumi wa mkoa kutokana na matarajio ya kupokea maelfu ya wageni watakaotumia huduma za malazi, usafiri, chakula, utalii na biashara nyingine mbalimbali.

Sitta alisema Tosamaganga ni shule ya kihistoria yenye usajili namba moja nchini (S1), jambo linaloifanya kuwa sehemu muhimu ya historia ya elimu Tanzania.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Tosamaganga, Laurent Manga, alisema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kumshukuru Mungu kwa mafanikio ya shule, kuwakutanisha wanafunzi wa zamani na wadau pamoja na kuhamasisha michango kwa ajili ya kuiboresha taasisi hiyo.

Alisema serikali imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya shule hiyo baada ya kutoa zaidi ya shilingi milioni 650 kwa ajili ya ukarabati wa majengo, hatua iliyowezesha wanafunzi kusoma katika mazingira salama na bora zaidi.

Manga alisema kutokana na matokeo mazuri ya kitaaluma, shule hiyo imepewa hadhi ya kuwa shule maalumu (Special School), ambapo sasa inapokea wanafunzi wa kidato cha tano wenye ufaulu wa juu wa alama za pointi 7 hadi 10.

Aidha alisema shule inaendelea kupata huduma muhimu zikiwemo maji, umeme na chakula bila changamoto kubwa, huku akitoa wito kwa wanafunzi wote wa zamani kurejea kushiriki maadhimisho hayo na kuchangia maendeleo ya shule.

“Tunatamani kupata basi la shule ili kuwasaidia wanafunzi katika shughuli mbalimbali za masomo na safari. Hili ni moja ya vipaumbele vyetu katika maadhimisho haya ya miaka 100,” alisema Manga.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Habari, Hamasa na Matangazo ya maadhimisho hayo, Mwalimu Gayrus Edward Mwakavindi, alisema kamati imeweka lengo la kukusanya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema michango inaweza kutumwa kupitia akaunti ya CRDB yenye jina la Tosa Maganga Jubilee pamoja na njia nyingine za malipo zilizotengwa kwa ajili ya zoezi hilo.

Mwakavindi alisema kamati ya maandalizi imejumuisha walimu waliowahi kufundisha Tosamaganga, wanafunzi wa zamani wa vipindi mbalimbali, viongozi wa serikali, wanasiasa, wanamichezo na wadau wengine wenye mapenzi na shule hiyo.

Aliwahimiza waandishi wa habari kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhamasisha wananchi kushiriki maadhimisho hayo ili kuhakikisha historia ya miaka 100 ya Shule ya Sekondari Tosamaganga inaenziwa na kuacha alama kwa vizazi vijavyo.