Diwani wa Kata ya Kalangalala katika Manispaa ya Geita
ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Reuben Sagayika, amehitimu
mafunzo ya utawala, uongozi na maendeleo yaliyoandaliwa na Serikali ya China na
kuwashirikisha washiriki kutoka nchi 23 za ukanda wa Bahari ya Hindi.
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa takribani wiki tatu, yamefanyika
katika Yunnan International Center for Economic and Technical Exchange jijini
Kunming, China, na kuratibiwa na Wizara ya Biashara ya Jamhuri ya Watu wa
China.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti cha kuhitimu mafunzo
hayo, Sagayika amesema amepata fursa ya kujifunza namna China inavyotumia
mifumo bora ya utawala, uongozi na mipango ya muda mrefu katika kuchochea
maendeleo ya wananchi.
Amesema miongoni mwa mambo aliyojifunza ni umuhimu wa kuwa
na uongozi madhubuti, nidhamu na uwajibikaji, pamoja na kuwa na maono ya muda
mrefu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Sagayika amesema pia amejifunza umuhimu wa kuimarisha
taasisi za serikali, kuwekeza katika viwanda, miundombinu, teknolojia na
rasilimali watu, akibainisha kuwa maendeleo ya vijijini ni sehemu muhimu katika
kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi.
Kwa upande wa Tanzania, Sagayika amesema uzoefu alioupata
nchini China unaweza kutumika kama fursa ya kuboresha mifumo ya maendeleo kwa
kuzingatia mazingira, uwezo na mahitaji ya Tanzania.
Aidha, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na China
unaendelea kuwa na umuhimu katika kutoa fursa za biashara, uwekezaji,
teknolojia pamoja na ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu.
Sagayika amesema atashirikisha maarifa na uzoefu alioupata
katika mafunzo hayo na wadau mbalimbali nchini, ili yaweze kuchangia katika
kuboresha utawala, uongozi na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Post a Comment