" MKAKATI WA TAIFA WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA WAANZA KUTEKELEZWA MKINGA

MKAKATI WA TAIFA WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA WAANZA KUTEKELEZWA MKINGA





📌*Mitungi ya gesi ya kilo sita 3,255 kuuzwa kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 17,500*


📍*Mkinga, Tanga*

Serikali imeanza kutekeleza kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga, kupitia mradi wa usambazaji na uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku.


Kupitia mradi huo, jumla ya mitungi 3,255 ya gesi ya kilo sita itasambazwa na kuuzwa kwa wananchi wa Mkinga kwa bei ya ruzuku ya Shilingi 17,500 kwa mtungi.


Mwananchi anayehitaji kunufaika na mpango huo anatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA). Mtungi huo utauzwa ukiwa tayari kwa matumizi, ukiwa na gesi pamoja na vifaa muhimu.


Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.


Utekelezaji wa mradi huo unalenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi, salama na rafiki kwa afya na mazingira, huku ukipunguza utegemezi wa nishati zinazoweza kuwa na madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.


Wananchi wa Mkinga wameishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi huo.


Aidha, wameipongeza REA kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha unawafikia walengwa, hususan wananchi wa kipato cha chini.


Wamesema mradi huo utawasaidia kupata nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, jambo litakalosaidia kuboresha afya, kuhifadhi mazingira na kuongeza ubora wa maisha ya wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post