Mtoto Xyleen Mapunda (15) amesema amefurahi kujifunza namna madini ya urani yanavyotumika kutengeneza nishati ya nyuklia na faida zake alipowasili kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam akitoka nchini Urusi alikokwenda kwa safari ya kielimu na kisayansi baada ya kushinda Shindano la kimataifa la Icebreaker of Knowledge 2026 kupitia programu ya Kampuni ya Nishati ya Nyuklia ya Urusi, Rosatom.
Xyleen ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kufika Ncha ya Kaskazini katika safari ya siku 10 akiwa na wanafunzi wenzake wenye vipaji kutoka nchi 22 duniani, wakisafiri kutoka mji wa Murmansk kwenda Ncha ya Kaskazini, Franz Josef Land na kurejea Murmansk kwa kutumia meli kubwa zaidi duniani inayotumia nishati ya nyuklia ya 50 Let Pobedy.
Akizungumzia uzoefu wake, Xyleen amesema meli hiyo inatumia nyuklia na wamejifunza kwa vitendo namna madini ya urani yanavyotumika kutengeneza nishati hiyo na matumizi yake mbalimbali, jambo ambalo alieleza kuwa ni zuri na halikuwahi kuingia kwenye mawazo yake hapo awali.
Alisema kuwa kushiriki katika safari hiyo kulimpa furaha kubwa alipofikiria kuwa yeye ndiye mtoto wa kwanza kutoka Tanzania kufika kwenye ncha ya dunia, huku akisisitiza kuwa mafanikio hayo yanathibitisha kuwa haijalishi mtu anatokea wapi bali jitihada na kujiamini ndizo zinazomfikisha mtu malengo yake, kwani yeye mwenyewe hakutarajia kushinda lakini alifanikiwa.
Xyleen aliongeza kuwa safari hiyo si ya kwanza wala ya mwisho kwake kushiriki na kushinda, akitoa wito kwa wengine kujaribu na kujiamini kwa kuwa ushindi huanza na mtu mwenyewe kabla ya kuaminiwa na wengine.
Kwa mujibu wa Kampuni ya Rosatom, safari hiyo iliweka historia kama msafara wa 200 wa meli ya uso wa bahari kufika Ncha ya Kaskazini, ambapo haikuwa ya kutalii pekee bali iliambatana na programu maalumu ya elimu na tafiti zilizowakutanisha wanafunzi na wanasayansi katika mazingira halisi ya Arctic.
Miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni pamoja na majaribio ya kisayansi kama kurusha radiosonde kwa ajili ya mawasiliano katika maeneo magumu na majaribio ya jukwaa linaloweza kurejeshwa kutoka tabaka la stratosphere, huku washindi wakipitia hatua tatu za mashindano yaliyowapima katika masomo ya sayansi, nishati ya nyuklia, uchunguzi wa Arctic na ubunifu wa miradi inayohusu teknolojia za nyuklia zinazobadilisha dunia.
Nahodha wa meli hiyo, Ruslan Saso, alisema safari hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa katika kuwajengea kizazi kipya hamasa ya kujifunza, kufanya tafiti na kutimiza ndoto zao za kisayansi.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment