" SHINYANGA: MWENGE WA UHURU WAZINDUA TAWI JIPYA LA CRDB TINDE, WANANCHI ZAIDI YA 10,000 WAFUNGUA AKAUNTI

SHINYANGA: MWENGE WA UHURU WAZINDUA TAWI JIPYA LA CRDB TINDE, WANANCHI ZAIDI YA 10,000 WAFUNGUA AKAUNTI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenge wa Uhuru umezindua rasmi Tawi jipya la Benki ya CRDB Tinde, mkoani Shinyanga, katika hatua inayolenga kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi wa Tinde na maeneo jirani.

Tawi hilo lililopo Njiapanda ya Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, takribani kilomita 35 kutoka Shinyanga Mjini, limezinduliwa leo Alhamisi, Agosti 20, 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za CRDB kuongeza upatikanaji wa huduma za kibenki katika maeneo mbalimbali nchini.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza CRDB kwa kuendelea kupanua wigo wa huduma za kifedha na kuwekeza katika miundombinu inayowarahisishia wananchi kupata huduma hizo bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Mwang’onda pia amepongeza ushirikiano kati ya CRDB na Serikali katika utekelezaji wa programu mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi, ikiwemo utoaji wa mikopo kwa makundi mbalimbali pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii na michezo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mikopo wa CRDB, Xavery Makwi, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, amesema uwepo wa tawi hilo Tinde utasaidia kupunguza changamoto ya wananchi kusafiri hadi Shinyanga Mjini kwa ajili ya kupata huduma za kibenki.

Makwi amesema CRDB tayari imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 31 kwa makundi mbalimbali, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, watumishi, wastaafu na watu binafsi, huku akiwataka wananchi wa Tinde kutumia fursa zinazotolewa na benki hiyo kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Tawi la CRDB Tinde ni miongoni mwa matawi 25 ya benki hiyo katika Kanda ya Magharibi, inayohusisha mikoa ya Shinyanga, Tabora, Kigoma na Geita.

Ujenzi wa jengo hilo jipya ulianza mwaka 2016 na umehusisha uwekezaji wa shilingi milioni 650, zilizotumika katika ununuzi wa eneo, ujenzi wa jengo pamoja na uwekaji wa vifaa muhimu vya huduma za kibenki. Tawi hilo lilianza kutumia jengo hilo jipya mwezi Aprili 2026.

Taarifa za maendeleo ya huduma za tawi hilo zinaonesha kuwa tayari zaidi ya wananchi 10,000 wamefungua akaunti za benki kupitia Tawi la CRDB Tinde, jambo linaloashiria ongezeko la matumizi ya huduma rasmi za kifedha katika eneo hilo.

Baadhi ya wananchi wa Tinde na maeneo jirani wameipongeza CRDB kwa kusogeza huduma hizo karibu nao, wakieleza kuwa hatua hiyo imepunguza gharama na muda ambao walikuwa wakitumia kusafiri hadi Shinyanga Mjini kwa ajili ya huduma kama kuweka na kutoa fedha.

Uwepo wa tawi hilo pia unatarajiwa kuongeza fursa kwa wananchi kupata huduma za kifedha kwa urahisi zaidi na kuchochea ukuaji wa shughuli za biashara na uchumi wa kaya katika Tinde na maeneo yanayolizunguka.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi la CRDB Tinde.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi la CRDB Tinde mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi, akikabidhi taarifa ya mradi huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post