Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini Bw. Ndiame Diop, tarehe 20 Agosti, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti20,2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bw. Ndiame Diop.Mazungumzo yao yamelenga kuharakisha uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuchochea mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Katika mazungumzo hayo Rais Dkt. Samia ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake wa muda mrefu na Tanzania, hususan katika sekta za elimu, nishati, miundombinu na kilimo, na kutoa wito wa kuimarishwa zaidi kwa ushirikiano huo kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya muda mrefu vya Taifa. “Tunathamini mchango wa Benki ya Dunia katika maendeleo ya Tanzania. Tunapoingia katika hatua inayofuata ya mabadiliko yetu, kipaumbele chetu ni kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu unachochea uzalishaji wa uzalishaji, biashara, uwekezaji na ajira kwa vijana wetu,” amesema Rais Dkt. Samia.Mazungumzo hayo yamejikita katika Reli ya Kisasa (SGR), miundombinu ya usafirishaji na nishati inayounganisha nchi za ukanda, kilimo cha kisasa, uvuvi, elimu na maendeleo ya ujuzi, pamoja na fursa za kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi. Rais Dkt. Samia ameeleza nafasi ya kimkakati ya Tanzania kama lango linalounganisha Afrika Mashariki, Kati na Kusini, akisisitiza kuwa uwekezaji katika reli, bandari, barabara na nishati unapaswa kuimarisha mtangamano wa kikanda na wakati huo huo kufungua fursa mpya za kiuchumi katika Ushoroba wa Kati. “Mradi wa SGR ni zaidi ya reli. Tunauona kama ukanda wa kiuchumi wenye uwezo wa kuchochea viwanda, kilimo, shughuli za usafirishaji na ugavi, ukuzaji wa miji mipya na biashara ya kikanda. Tunataka kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zinazotokana na uwekezaji huu mkubwa,” amesema Rais Dkt. Samia.Katika kilimo, Rais Dkt. Samia amesisitiza dhamira ya Tanzania ya kuendeleza kilimo cha kisasa na cha kibiashara, kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, kwa kuimarisha umwagiliaji, matumizi ya teknolojia na mitabmo, uongezaji thamani na uhusiano imara zaidi na masoko. Viongozi hao pia wamejadili umuhimu wa sayansi, teknolojia, elimu ya ufundi na maendeleo ya ujuzi katika kuwaandaa vijana wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi unaobadilika kwa kasi. Kwa upande wake, Bw. Diop amepongeza hatua za maendeleo zinazopigwa na Tanzania na kuthibitisha dhamira ya Benki ya Dunia ya kuendelea kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.Bw. Diop ameonesha kuvutiwa hasa na maendeleo ambayo Tanzania imeyafikia kupitia mradi wa kusambaza umeme barani Afrika (Mission 300), ikiwemo juhudi za kuimarisha miundombinu ya nishati inayounganisha nchi za ukanda. Aidha, Bw. Diop amepongeza maendeleo katika sekta ya elimu, akitaja hatua alizozishudia Zanzibar, ikiwemo matumizi ya sayansi na teknolojia pamoja na uwekezaji unaolenga kuboresha ujifunzaji na kuwaandaa vijana kwa fursa za baadaye. “Tunachokiona katika maeneo kama nishati na elimu kinaonesha kile kinachoweza kufikiwa pale uwekezaji unapolenga matokeo ya maendeleo yenye tija,” amesema Bw. Diop.Mazungumzo hayo pia yamesisitiza nafasi ya sekta binafsi katika kufanikisha mabadiliko ya Tanzania. Bw. Diop ameeleza utayari wa Benki ya Dunia kusaidia Tanzania kuweka mazingira yatakayochochea ukuaji zaidi wa sekta binafsi, ikiwemo kuvutia mitaji binafsi na kusaidia uwekezaji wenye tija katika sekta za uzalishaji na miundombinu. Tanzania na Benki ya Dunia zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kubadili vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania kuwa uwekezaji wa kimkakati wenye uwezo wa kuharakisha ukuaji wa uchumi, kuimarisha mtangamano wa kikanda na kuleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini Bw. Ndiame Diop, tarehe 20 Agosti, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini Bw. Ndiame Diop, tarehe 20 Agosti, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254








Post a Comment