" Viongozi wa Siasa Wataka Tume ya Maridhiano iwalinde Watanzania na Kujenga Umoja wa Kitaifa

Viongozi wa Siasa Wataka Tume ya Maridhiano iwalinde Watanzania na Kujenga Umoja wa Kitaifa



Viongozi mbalimbali wa siasa nchini wametoa ushauri mzito kwa serikali kuhusu uundaji wa Tume ya Maridhiano, wakisisitiza kuwa jukumu lake kuu linapaswa kuwa ni kulinda amani, umoja, na mshikamano wa wananchi wote.

Ushauri huo umetolewa kufuatia tamko la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Julai 30, mwaka huu, ambapo alieleza kuwa serikali inatarajia kuunda tume hiyo ili kuharakisha mchakato wa marekebisho ya katiba wakati uchunguzi wa matukio ya uchaguzi ukiendelea.

Viongozi hao wameeleza kuwa mafanikio ya tume hiyo yatategemea sana namna itakavyowashirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta zote na kuweka maslahi ya taifa mbele badala ya maslahi binafsi ya wanasiasa.

Wakitoa maoni yao, wanasiasa wakongwe na aliyekuwa wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 wamesisitiza umuhimu wa uwazi, ushirikishwaji mpana, na kuzingatia misingi ya sheria na haki.

Hamad Rashid Mohammed amewahimiza viongozi kuzingatia masuala ya utaifa na demokrasia ili kuepusha migongano, huku Yustas Rwamugira akisisitiza kuwa amani na utulivu ndio msingi mkuu wa kila jambo na lazima vipewe kipaumbele cha juu kabisa.

Naye Salum Rashid alionya dhidi ya wanasiasa wenye ajenda za uchochezi na kushauri uwepo wa uwakilishi makini kutoka kwa vijana na mikoa iliyoathiriwa na vurugu ili kupata suluhu ya kudumu.

Aidha, viongozi wengine kama David Mwaijojele na Coaster Kibonde wamehimiza utamaduni wa uvumilivu, kusameheana, na kugusa makundi yote ya jamii yakiwemo ya walemavu, wanawake, na wafanyakazi badala ya kuwashirikisha wanasiasa pekee. Kwa upande wake, Kunje Ngombale Mwiru alisisitiza kuwa maridhiano hayapaswi kulenga maslahi ya kisiasa na madaraka pekee, bali yaangalie ustawi mpana wa huduma za jamii na maendeleo ya nchi.

Mtazamo huo unaungwa mkono na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo kupitia kwa Katibu wa NEC ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, kimesema kuwa maridhiano ni njia thabiti ya kujenga taifa imara kupitia mazungumzo na uvumilivu badala ya misimamo mikali.

Post a Comment

Previous Post Next Post